Shura ya Maimamu Tanzania yakaribisha kuachiwa huru Masheikh 12
Shura ya Maimamu Tanzania imepokea kwa mikono miwili uamuzi wa mahakama wa kuwaachia huru Masheikh 12 waliokaa gerezani miaka 10, (2015-2025), kwa tuhuma za ugaidi. Uamuzi huo umetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Mheshimiwa Arnold John Kirekiano.
Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP, aliambia Mahakama upande wa Jamhuri hauna haja ya kuendelea tena na shauri hilo. Akitoa uamuzi huo jana Machi 4, Mheshimiwa Jaji amesema amekubali ombi hilo la Mwendesha Mashtaka wa serikali.
Kwa muda mrefu, Shura ya Maimamu Tanzania imekua ikimuomba Mkurugenzi wa Mashtaka DPP kulifuta shauri hilo kwa sababu za upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya Masheikh hao.
Walioachiwa huru ni: Ali Mohammed Ulatule (70), Khamisi Mohammed Ulatule (61), Nassoro Suleiman Ulatule (41), Rajab Ali Mohammed Ulatule (34) na Ramadhani Khamisi Mohammed Ulatule (29).
Wengine ni: Saidi Abdallah Chambeta, Fadhili Shaabani Lukwembe, Mnemo Qassim Mwatumbo, Abdallah Bushiri kalukula, Khamisi Ally Masamba, Omari Abdallah Makota na Mohammed Hassan Ungando.
Katika kundi la Masheikh walioachiwa huruu, 5, ni wa familia moja ya Ulatule. Walikamatwa familia moja watu 16, na baada ya masiku kadhaa (ya kutofahamika walipo), hatimaye 7, walikutwa katika Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam baada ya kufikishwa Mahakamani na kusomewa shitaka la ugaidi.
Aidha wenzao 9, hawajulikani walipo mpaka leo. Kati ya 7, waliokua gerezani 2, Sheikh Suleiman Mohammed Ulatule (99), na Sheikh Saidi Mohammed Ulatule (79), wamefariki dunia wakiwa gerezani. Kufuatia kuachiwa kwa masheikh hao 12, idadi ya mahabusu wenzao waliobaki katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam ni 39.