Kwa nini Marekani inataka kuwekeza katika sekta ya madini nchini Kongo DR?
(last modified Wed, 12 Mar 2025 12:32:35 GMT )
Mar 12, 2025 12:32 UTC
  • Kwa nini Marekani inataka kuwekeza katika sekta ya madini nchini Kongo DR?

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Marekani zinapanga kushirikiana katika mapatano ya kiuchumi na kisiasa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilmetangaza kuwa, Washington, katika mkondo wa siasa za utawala wa Donald Trump, inakaribisha ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kufaidika na rasilimali za madini yenye thamani na muhimu za nchi hiyo.

Msimamo huu wa serikali ya Marekani umetangazwa baada ya maafisa wa Kongo kuwasiliana na wenzao wa Washington na kutaka kufikiwa makubaliano ya kuwekeza katika sekta ya madini ya nchi hiyo ya Kiafrika mkabala wa kudhaminiwa usalama na kuihami nchi hiyo katika vita dhidi ya waasi wa M23. 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi hivi karibuni alipendekeza ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya maliasili ya thamani ya Kongo kwa Marekani, katika juhudi za kukabiliana na waasi mashariki mwa Kongo.

Vita katika mipaka ya mashariki mwa Kongo vimepamba moto zaidi katika miezi ya hivi karibuni, na waasi wa M23 wamefanikiwa kuteka maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na miji miwili mikubwa ya mashariki mwa nchi. Suala hili limezidisha hatari ya vita kubwa katika eneo hilo la Maziwa Makuu ya Afrika, hasa kwa vile nchi jirani kama Rwanda pia  zinatuhumiwa kwamba zinahusika katika vita hivyo kwa kuwasaidia waasi wa M23.

Nchi ya Kongo hususan mashariki mwa nchi hiyo, imejaa madini na utajiri mkubwa wa kimaumbile ambao unakodolewa macho na nchi mbalimbali kwa miongo kadhaa, na suala hilo linahesabiwa kuwa moja ya sababu za vita vya sasa mashariki mwa nchi hiyo. 

Kongo inasifika kwa kuwa na akiba kuubwa ya madini ya aina mbalimbali.

Ripoti zilizochapishwa zinaonyesha kuwa, rasilimali hizo ni pamoja na shaba, dhahabu, almasi, titanium, na madini mengine ambayo ni muhimu sana kwa tasnia na teknolojia mpya. Nchi hiyo pia ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa cobalt duniani, ambayo ni mada muhimu kwa utengenezaji wa betri za lithiamu-ion, ambazo hutumika katika magari ya umeme na simu za rununu. Vilevile kutokana na kukua kwa mwenendo wa matumizi ya teknolojia duniani hasa viwandani na sisitizo la kupunguzwa utegemezi kwa nishati ya mafuta ya petroli, mahitaji ya cobalt na metali nyingine zikiwemo shaba na titanium, yameongezeka. Katika suala hili, Marekani, kama moja ya watumiaji wakubwa na wazalishaji wa teknolojia mpya, inahitaji migodi na rasilimali hizi zaidi kuliko hapo awali.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema kuhusiana na sula hilo kwamba: "Kongo ina sehemu kubwa ya madini muhimu duniani yanayohitajika katika teknolojia ya kisasa, na serikali ya Marekani imechukua hatua za kuimarisha uwekezaji wa sekta binafsi wa Marekani huko DRC ili kufaidika na rasilimali za madini."

Katika hali hii, kupamba moto vita na machafuko mashariki kwa Kongo DR kumetayarisha mazingira mwafaka kwa Marekani kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kufunga mikataba yenye faida na kuwepo zaidi katika kanda hiyo kuliko hapo awali. Washington daima imekuwa ikifanya mikakati ya kuzidisha uwepo wake katika eneo hilo la Afrika, si tu kwa sababu ya kunufaika na madini na utajiri wa nchi za kanda hiyo tu, bali pia kwa sababu inalenga kushindana na makampuni ya China yaliyoko katika bara hilo, kuzidisha ushawishi wa Washington na kurahisisha biashara na uhusiano wa kibiashara na Afrika.  

Marekani inataka kushindana na China barani Afrika

Kwa upande mwingine, inaonekana kwamba sera ya "nipe madini nikudhaminie usalama" katika kipindi kipya cha urais wa Trump, sambamba na kauli mbiu yake ya "Marekani Kwanza", imepewa uzito mkubwa zaidi, kama ilivyobainika pia hivi karibuni katika jitihada za Trump za kutaka kusaini mkabala wa usalama mkabala wa madini na nchi ya Ukraine. Trump, ambaye ana historia ndefu katika nyanja za shughuli za kiuchumi na kibiashara, anataka kunyonya migodi yenye thamani kubwa duniani kote katika utawala wake kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi ya Marekani au makampuni ya nchi hiyo. Katika mkondo huo, anatumia masuala ya kulinda usalama kwa ajili ya kudhibiti sehemu kubwa ya masoko ya kimataifa yajayo kwa kupata umiliki au hisa kubwa ya migodi ya madini hasa madini adimu, ili kuimarisha nafasi ya Marekani duniani.

Hata hivyo, nchi kama Kongo sasa zinataka kufikia makubaliano na Washington ndani ya fremu ya kutoa mali mkabala wa kupewa dhamana ya usalama, bila kujali matokeo mabaya ya kukubali uwepo wa majeshi ya Marekani katika ardhi ya nchi hiyo, wakati uzoefu wa awali unaonyesha kuwa, Washington haijawahi kutimiza ahadi wala kutekeleza makubaliano yake na nchi nyingine katika suala hili.