Msaada unatakiwa kuzisaidia nchi za Kusini mwa Afrika zilizoathiriwa na ukame
(last modified Mon, 01 Aug 2016 07:25:45 GMT )
Aug 01, 2016 07:25 UTC
  • Msaada unatakiwa  kuzisaidia nchi za Kusini mwa Afrika zilizoathiriwa na ukame

Mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu kusini mwa Afrika yameomba kusaidiwa kiasi cha dola bilioni moja ili kukabiliana na janga la ukame lililoziathiri baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika.

Mashirika hayo yameeleza kuwa eneo la kusini mwa bara la Afrika limeathiriwa na hali ya hewa ya El Nino ambayo huathiri unyeshaji mvua na kisha kuvuruga shughuli za kilimo. Nchi hizo za Kusini mwa bara la Afrika zinakabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kualiathiri eneo  hilo katika kipindi cha miaka 35 ya hivi karibuni. 

Ripoti zinasema kuwa ukame huo unatishia maisha ya watu milioni 12 na laki tatu wa kusini mwa Afrika. Hii ni kwa sababu watu hao sasa wameishiwa na akiba zao za chakula huku wakitaabika na kusindwa hata kujidhaminia huduma za msingi kabisa kama maji. 

Baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika zilizoathiriwa na janga la ukame 
 

 Angola, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Swaziland, Zimbabwe, Madagascar ni nchi zilizoathirika pakubwa na janga la ukame katika eneo la kusini mwa bara la Afrika; kiasi kwamba  katika baadhi ya maeneo ya nchi hizo mito na mabwawa yamekauka, ardhi za kilimo zimeharibika na mifugo kuaga kwa kukosa maji na malisho.

Wakati huo huo Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) Alhamisi iliyopita liliomba kupatiwa msaada wa haraka wa kilimo wa dola milioni moja na tisa kwa ajili ya nchi kumi za kusini mwa Afrika ambazo zimeathiriwa vibaya na ukame.