Afrika Kusini iliwafukuza karibu wahamiaji haramu 47,000 mwaka wa fedha wa 2024/25.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini imetoa ripoti mpya na kusema kuwa, Pretoria iliwafukuza wahamiaji haramu 46,898 mwaka wa fedha wa 2024/25.
Idadi hiyo inaashiria ongezeko la asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita, ambapo wahamiaji haramu 39,672 walifukuzwa nchini Afrika Kusini.
Katika taarifa yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini, Leon Schreiber amesema: "Ongezeko hili kubwa la ufanisi wa utekelezaji linaonyesha dhamira yetu ya kuzingatia utawala wa sheria."
Ameongeza kuwa, takwimu za kurejeshwa makwao wahamiaji haramu katika mwaka wa fedha wa 2024/25 ni za juu zaidi ikilinganishwa kwa uchache na miaka mitano iliyopita. Kwa mujibu wa takwimu za idara hiyo, wahamiaji haramu 22,560 walifukuzwa katika mwaka wa fedha wa 2022/23, 20,093 mwaka 2021/22, na 14,859 mwaka 2020/21.
Amesema: "Utendaji huu ulioboreshwa, pamoja na mageuzi yetu ya kidijitali ambayo yanadhibiti kuingia na kutoka yataendelea kuzuia watu kuingia nchini kinyume cha sheria kupitia bandari zetu, na yote hayo yanachangia kuimarishwa usalama wa taifa na uwezeshaji wa biashara."
Wachimba migodi haramu huwa wanaingia Afrika Kusini kutoka duniani kote kutafuta fursa bora zaidi. Polisi wamekuwa wakiweka vizuizi barabarani ili kubaini wageni wasio na vibali, huku baadhi ya watu wakikamatwa wakati wa operesheni za kawaida za kuwasimamisha, kuwasaili na baadaye kuwakamata.