Wananchi wa Morocco waandamana kulaani jinai za Israel Gaza
(last modified Mon, 07 Apr 2025 11:36:46 GMT )
Apr 07, 2025 11:36 UTC
  • Wananchi wa Morocco waandamana kulaani jinai za Israel Gaza

Maelfu ya wananchi wa Morocco wamefanya maandamano makubwa katikati mwa mji mkuu wa Rabat kulaani mashambulio mapya ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji hao walikusanyika karibu na majengo ya Bunge, wakipeperusha bendera za Palestina, huku wakipiga nara za mshikamano na wananchi madhulumu wa Palestina,

Kadhalika wametaka kusitishwa mara moja mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza, huku wakitoa wito kwa mamlaka za Morocco kukata uhusiano wote wa kisiasa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Maandamano hayo ya jana Jumapili yaliandaliwa na 'Jumuiya ya Morocco ya Kuisaidia Palestina na Kupinga Uhusiano wa Kawaida na Israel', pamoja na makundi mengine kadhaa ya haki za binadamu ya nchi hiyo.

Washiriki wa maandamano hayo, huku wakitangaza mshikamano na taifa la Palestina, wametoa mwito wa kuendelea kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na kulaani vikali kulengwa kwa wafanyakazi wa sekta ya tiba na waandishi wa habari huko Gaza.

Wamorocco wakiwa wamebeba bendera za Palestina mjini Rabat

Morocco ilikuwa nchi ya nne ya Kiarabu kukubali kurejesha uhusiano na Israel mwaka 2020 baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan.

Hata hivyo wananchi wa Morocco kama wenzao katika nchi nyingine za Kiarabu wamekuwa wakiandamana kupinga vikali uamuzi wa serikali zao kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel; na wametaka mapatano ya kuanzisha uhusiano huo yafutwe.