Asasi za kiraia, wapinzani Tanzania walaani kukamatwa Tundu Lissu
(last modified Fri, 11 Apr 2025 12:32:57 GMT )
Apr 11, 2025 12:32 UTC
  • Asasi za kiraia, wapinzani Tanzania walaani kukamatwa Tundu Lissu

Mashirika ya kiraia, vyama vya upinzani na asasi za kutetea haki za binadamu nchini Tanzania zimekosoa vikali hatua ya kukamatwa na kushtakiwa Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo CHADEMA.

Mashirika hayo na vyama vya upinzani vimeishutumu serikali kwa kuwawekea mbinyo wapinzani kuelekea uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Serikali ya Dar es Salaam imekanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa mashtaka dhidi ya Lissu yanatokana na misingi ya sheria, kwa kuwa mwanasiasa huyo anachochea uasi na kushajiisha kususiwa uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Lissu alipandishwa kizimbani jana Alkhamisi kwa tuhuma za uhaini; shitaka ambalo hukumu yake ni kifo, kwa matamshi yake aliyoyatoa wiki iliyopita ambayo waendesha mashtaka walisema alitoa wito kwa umma kuanzisha uasi na kuvuruga uchaguzi ujao.

Mashtaka yanayomkabili Lissu, ambaye ni mshindi wa pili katika uchaguzi wa urais wa 2020, yameibua upya rekodi ya haki za binadamu ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati huu anafanya kampeni ya kuchaguliwa tena.

Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan

Wakili wa mwanasiasa huyo ambaye alinusurika jaribio la mauaji mwaka 2017 baada ya kumiminiwa risasi na watu wasiojulikana, Rugemeleza Nshala, amepuuzilia mbali mashtaka hayo akisema yalichochewa kisiasa.

"Hii ni (kesi) ya kisiasa tu. Mteja wangu alikuwa akizungumza na wafuasi wa chama chake na kueleza msimamo wa chama kuhusu mageuzi ya uchaguzi," aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama.

Chadema imeendelea kushinikiza mageuzi makubwa ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi. Chama hicho kimeonya kuwa, huenda kikasusia uchaguzi iwapo mageuzi hayo hayatapasishwa.