CHADEMA yataka Lissu aruhusiwe kuonana na mawakili, jamaa zake
(last modified Sat, 19 Apr 2025 06:30:59 GMT )
Apr 19, 2025 06:30 UTC
  • CHADEMA yataka Lissu aruhusiwe kuonana na mawakili, jamaa zake

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA kimevitaka vyombo vya dola vimruhusu Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Tundu Lissu kuonana na mawakili na jamaa zake.

Katika taarifa Ijumaa hii, CHADEMA kupitia Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia imekosoa vikali hatua ya Lissu kuzuiliwa katika sehemu isiyojulikana. Chama hicho kimesema mwanasiasa huyo ana haki ya kikatiba ya kuruhusiwa kuonana na mawakili na watu wa familia yake. Duru za habari zinasema Lissu anashikilia katika Gereza la Keko visiwani Zanzibar.

Wanaharakati wa kutetea haki na vyama vya upinzani wameituhumu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba inazidisha ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu; tuhuma ambazo serikali hiyo inazikanusha.

Hayo yanajiri huku Mwenyekiti huyo wa Chadema akiendelea kusota mahabusu baada ya kukamatwa na kushtakiwa kwa kosa la uhaini kwa kile waendesha mashtaka wa serikali walichosema kuwa ni hotuba yake ya kuwataka wananchi kuanzisha uasi na kuvuruga uchaguzi. Hapo awali CHADEMA ilitishia kususia na kuzuia kufanyika uchaguzi endapo hayatafanywa mageuzi makubwa katika sheria za uchaguzi ambazo inasema zinakipendelea chama tawala CCM.

Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema kuwa madai ya kubadilishwa kwa mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 hayawezi kutekelezwa kwa kipindi kifupi kilichobaki kwani mabadiliko makubwa yameshafanyika ikiwemo kuunda Tume Huru inayojitegemea

Amesema mapungufu ya mabadiliko hayo yanapaswa kupimwa baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika.  Simbachawene ameeleza kuwa mchakato unaogusa katiba ni suala linalohitaji muda, rasilimali, na ushirikishwaji mpana wa wananchi na sio kikundi cha watu fulani.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (INEC) ilitangaza Jumamosi ya wiki iliyopita kuwa CHADEMA haitaweza kushiriki katika katika uchaguzi wa urais na ubunge unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu baada ya kukataa kutia saini hati ya maadili ya uchaguzi iliyoandaliwa na tume hiyo. Hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Rugemeleza Nshala amesema: “Haki ya kikatiba haiwezi kuondolewa kwa kanuni za maadili zilizoundwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi”.