Misri na Djibouti zalaani mashambulizi mapya ya Israel katika Ukanda wa Gaza
(last modified Thu, 24 Apr 2025 10:47:57 GMT )
Apr 24, 2025 10:47 UTC
  • Misri na Djibouti zalaani mashambulizi mapya ya Israel katika Ukanda wa Gaza

Rais wa Misri, Abdel-Fattah al-Sisi na mwenzake wa Djibouti, Ismail Omar Guelleh wametangaza uungaji mkono wao kwa juhudi za kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza, na kulinda usalama wa baharini katika Bahari Nyekundu.

Shirika la habari la Xinhua limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, "Marais hao wawili wamelaani uvamizi mpya wa Israel katika Ukanda wa Gaza, ambao unaashiria ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano." 

Taarifa ya pamoja ya marais hao hao baada ya kumalizika mkutano wao nchini Djibouti imesema: Wawili hao wamesisitiza uungaji mkono wao kwa maazimio ya mkutano wa dharura wa kilele wa nchi za Kiarabu kuhusu Palestina uliofanyika nchini Misri Machi 4, ambao ulisisitiza haja ya usitishaji vita mara moja Gaza na kuasisiwa taifa huru la Palestina kwenye mipaka ya 1967, huku Quds ukiwa mji mkuu wake.

Kuhusu usalama wa Bahari ya Sham, Marais wa Misri na Djibouti wamepinga majaribio yoyote ya kutishia usalama na uthabiti wa njia za baharini," wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu kati ya mataifa ya Kiarabu na Afrika yanayopakana na Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden.

Wametoa wito wa kuanzishwa Baraza la Nchi za Kiarabu na Afrika zinazopakana na Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden litakalopewa jukumu la kupiga jeki uratibu na ushirikiano wa kikanda, na kuzingatia sheria za kimataifa za baharini.

Kadhalika Marais hao wawili wametangaza kuunga mkono juhudi za kurejesha umoja, amani na utulivu katika mataifa ya Kiarabu yanayokabiliwa na migogoro, hususan Sudan, Syria na Yemen.