RSF yaendelea kuua raia Sudan, UN yasema milioni 13 wamelazimika kukimbia makazi yao
(last modified Fri, 25 Apr 2025 13:47:12 GMT )
Apr 25, 2025 13:47 UTC
  • RSF yaendelea kuua raia Sudan, UN yasema milioni 13 wamelazimika kukimbia makazi yao

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema watu 11 wameuawa na 22 kujeruhiwa wakati ndege isiyo na rubani ya Rapid Support Forces (RSF) iliposhambulia kambi ya wakimbizi huko Atbara, kaskazini mwa Sudan.

Haya yanajiri huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) likisema kuwa takriban watu milioni 13 nchini Sudan wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita.

Vyanzo vya ndani vya Sudan pia vimesema kwamba ndege zisizo na rubani zimeshambulia maeneo ya mji wa kaskazini wa Atbara, na kusababisha kukatika kwa umeme katika mji huo.

Shirika la Umeme la Sudan limesema kwamba kituo cha transfoma cha Atbara kimeshambuliwa na ndege zisizo na rubani leo Ijumaa, suala lililosababisha hitilafu ya umeme katika majimbo ya Mto Nile na Bahari Nyekundu.

Shambulio hili ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi ya hivi karibuni ya ndege zisizo na rubani zilizolenga vituo vya umeme katika miji ya kaskazini mwa Sudan, ikiwa ni pamoja na Merowe, Dongola, Al Dabbah na Atbara.

Serikali ya Sudan mara kwa mara imekuwa ikiwatuhumu wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) kuwa ndio wanaohusika na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye mitambo ya kuzalisha umeme na miundombinu.

Kwa upande wa masuuala ya kibinadamu, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya kwamba linakabiliwa na uhaba wa fedha ambao unaweza kuathiri uwezo wake wa kutoa msaada kwa wale wanaosumbuliwa na uhaba mkubwa wa chakula nchini Sudan, ndani ya wiki.

Shirika hilo linalenga kuchangisha dola milioni 698 kusaidia watu milioni 7 kuanzia Mei hadi Septemba mwaka huu.