Washukiwa wa al-Shabaab waua Wakenya watano Mandera
(last modified Wed, 30 Apr 2025 02:33:11 GMT )
Apr 30, 2025 02:33 UTC
  • Washukiwa wa al-Shabaab waua Wakenya watano Mandera

Wafanyakazi watano wa machimbo wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa wakati gari lao liliposhambuliwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigadi la al-Shabaab kaskazini mashariki mwa Kenya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watu wapatao 10 waliokuwa wamejizatiti kwa silaha na wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia, walivamia basi dogo lililokuwa limebeba wafanyakazi hao alfajiri ya jana karibu na kijiji cha Bur Abor katika Kaunti ya Mandera.

"Wafanyakazi hao waliagizwa kukabidhi simu zao za rununu na vitambulisho na baada ya kuarishwa kushuka kwenye gari hilo. Katika harakati hizo (waliuawa kwa kupigwa risasi wakiwa wamelala chini," ripoti ya polisi imesema.

Inaarifiwa kuwa, magaidi hao walikimbia na kuelekea upande wa mpaka wa Somalia baada ya kutekeleza unyama huo. Habari zaidi zinasema kuwa, wafanyakazi 13 walinusurika kifo baada ya kutorokea msituni na baadaye kuokolewa.

Magaidi wa al-Shabaab wamekuwa wakiendesha uasi dhidi ya serikali ya Somalia tangu mwaka 2007, wakitaka kutwaa mamlaka na kuanzisha utawala kwa kuzingatia tafsiri yao kali ya sheria za Kiislamu.

Kundi hilo la kigaidi lenya mfungamano na mtandao wa al-Qaeda, mara nyingi huvuka mpaka na kuingia nchini Kenya kufanya mashambulizi.

Genge hilo linadai kuwa linafanya hujuma hizo dhidi ya maafisa usalama na raia wa Kenya kwa kuwa nchi hiyo ndio mchangiaji mkubwa wa wanajeshi katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.