Jeshi la Somalia laangamiza magaidi 17 wa al-Shabaab
Wizara ya Ulinzi wa Somalia imesema kwamba, Jeshi la Kitaifa la nchi hiyo limewaua magaidi 17 wa al-Shabaab katika operesheni ya anga iliiyofanyika kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na wizara hiyo imeeleza kuwa, operesheni hiyo ililenga maficho ya magaidi hao katika eneo la Jabad Godone katika jimbo la Shabelle ya Kati, ambapo kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda lilikuwa linapangia mashambulizi na kutengeneza mada za miripuko.
Imeongeza kuwa operesheni hiyo, iliyofanywa kwa usaidizi wa vikosi vya kimataifa, iliharibu silaha na magari yaliyokuwa yanatumiwa na kundi hilo la kigaidi katika operesheni zake.
Al-Shabaab imekuwa ikiendesha uasi dhidi ya serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16, na mara kwa mara imekuwa ikilenga vikosi vya usalama, maafisa wa serikali, na raia.
Tangu mwishoni mwa 2024, Jeshi la Kitaifa la Somalia na vikosi vya usalama katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland vimeshadidisha mashambulizi ya anga dhidi ya al-Shabaab katika majimbo ya kusini na kati, na dhidi ya ISIS (Daesh) katika eneo la Bari la kaskazini mashariki, kwa ushirikiano na washirika wa usalama wa kimataifa.
Haya yanajiri huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia akisisitiza kuwa, hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kulitambua eneo lililojitenga la Somaliland kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya nchi yake.
Serikali ya Mogadishu imeeleza kuwa, lengo la Israel la kulitambua eneo la Somaliland ni kuigawa vipande vipande Somalia, na kuyashajiisha makundi ya kigaidi nchini humo.