Wanawake wa Morocco wadai usawa katika kazi za nyumbani, wataka wanaume nao wavae "aproni" za jikoni
(last modified Fri, 02 May 2025 07:15:30 GMT )
May 02, 2025 07:15 UTC
  • Wanawake wa Morocco wadai usawa katika kazi za nyumbani, wataka wanaume nao wavae

Kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, makumi ya wanawake wa Morocco wamefanya maandamano kwenye mitaa ya Casablanca wakisisitiza umuhimu wa kazi za nyumbani zisizo na malipo na kudai usawa wa kijinsia katika kugawana kazi za nyumbani.

Katika maandamano hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Changamoto kwa Usawa na Uraia kwa ushirikiano na Shirikisho la Wafanyakazi, wanaume na wanawake walishiriki wakiwa wamevalia vazi la jikoni (aprons) na kutoa kauulimbiu zinazotaka kugawanywa kazi za nyumbani kwa usawa baina ya wanawake na wanaume.

Rais wa chama hicho, Bushra Abdo, ameeleza kuwa "kazi za nyumbani ni shughuli muhimu na yenye thamani kubwa, katika suala la tija na thamani ya mali. Ameongeza kuwa takwa la chama hicho ni wanaume kushiriki kazi za nyumbani, akisisitiza kuwa jambo hilo halidhoofishi uanaume wa mwanaume au kupunguza thamani ya mwanamke; Kinyume chake, ni jitihada muhimu inayochangia utulivu na ustawi wa familia."

Mwaka jana, Morocco ilikaribia kupitisha sheria ya familia ambayo inakiri kwamba kazi za nyumbani zinazofanywa na mke ni kazi zisizofanywa bila kulipiwa ujira wake, lakini zinachangia kuzalisha mali ya pamoja wakati wa ndoa.