Kambi ya upinzani Kenya yapinga uteuzi wa Rais Ruto wa makamishna wa IEBC
-
Erastus Edung Ethekon
Ripoti kutoka Kenya zinasema, watu watano kati ya saba walioteuliwa na Rais William Ruto kusimamia Uchaguzi Mkuu ujao wana uhusiano wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja na kiongozi huyo pamoja na mshirika wake katika Serikali Jumuishi, Raila Odinga, hali ambayo imezua malalamiko kutoka kambi ya upinzani kwamba walioteuliwa hawatakuwa maamuzi huru.
Ripoti hizo zinasema baadhi ya wateule hao wa Rais Ruto walikuwa washirika wake wa kisiasa hapo awali, mmoja akiwa mshauri wa kisheria wa chama cha zamani cha ANC kilichoasisiwa na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi.
Itakumbwa kuwa, Alkhamisi iliyopita Rais William Ruto alimteua Erastus Edung Ethekon, aliyekuwa wakili wa Kaunti ya Turkana, kuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Pia aliteua Msajili wa Vyama vya Siasa Ann Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Profesa Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah kuwa makamishna wa tume hiyo.
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, tayari amemkosoa Rais Ruto akidai kuwepo upendeleo katika uteuzi huo. “Tuna wasiwasi mkubwa kwamba Bw Ruto ameteua maafisa hao kwa upendeleo kwa kupuuza kanuni ya mashauriano na makubaliano katika aliowapendekeza kuwa Mwenyekiti na makamishna wa IEBC."

Musyoka amesema: "Hatua hii imeunda taasisi isiyoaminika moja kwa moja. Kama tulivyosema katika mawasiliano ya awali kuhusu suala hili, sasa ni dhahiri kuwa nia ni kuiba si tu uchaguzi mkuu ujao bali pia chaguzi ndogo zijazo.”
Kalonzo Musyoka ameahidi kwamba taarifa ya kina kutoka kambi ya upinzani itatolewa Jumatatu ijayo.
Erastus Edung Ethekon ambaye ameteuliwa na Rais William Ruto kuwa mwenyekiti mpya wa IEBC ni mshirika wa karibu wa Naibu Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais Ruto, Josephat Nanok.