Kadhaa wauawa katika shambulio la droni kusini ya Sudan
(last modified Fri, 16 May 2025 07:06:44 GMT )
May 16, 2025 07:06 UTC
  • Kadhaa wauawa katika shambulio la droni kusini ya Sudan

Watu kadhaa wameripotiwa kuuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa, baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia hospitali moja katika mji wa El-Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini kusini mwa Sudan jana Alkhamisi.

Mashuhuda wameiambia Anadolu kwamba, droni hiyo ilishambulia Hospitali ya Kijeshi, yenye uhusiano na jeshi la Sudan. Bila kutaja idadi kamili, mashuhuda hao wameongeza kuwa, shambulio hilo limesababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Ingawaje hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, lakini inaaminika kuwa limefanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF). 

Siku ya Jumatano, Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulitangaza kuwa raia wanne wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa kwa shambulio la mizinga lililotekelezwa na RSF kwenye mji huo wa El-Obeid.

Aidha haya yanajiri siku chache baada ya Jeshi la Sudan kusema kwamba, wapiganaji wa kundi la waasi wa RSF wameua raia saba kwa shambulizi la makombora huko El-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan siku ya Jumatatu.

Kadhalika Jumamosi ilyopita, serikali ya Sudan iliituhumu RSF kwa kuua watu 21 na kuwajeruhi wengine 47 katika shambulio la angani kwenye Gereza la El-Obeid, kusini mwa Sudan.

Jeshi la Sudan limekuwa likipambana na waasi wa RSF tangu Aprili 2023, na vita hivyo vimepelekea vifo vya maelfu ya watu na kusukuma Sudan katika moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu 20,000 wameuawa na milioni 15 wamekimbia makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa na za ndani.