Ethiopia yataka matumizi mazuri ya AI kwa ajili ya maendeleo Afrika
(last modified Mon, 19 May 2025 03:10:20 GMT )
May 19, 2025 03:10 UTC
  • Ethiopia yataka matumizi mazuri ya AI kwa ajili ya maendeleo Afrika

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametoa mwito kwa nchi za Afrika kufanya jitihada za pamoja za kutumia vizuri Akili Mnemba (AI) nyumbani ili kutia nguvu ustawi na maendeleo ya bara hilo.

Abiy amesema hayo alipokuwa anahutubia mkutano wa ngazi ya juu ambao maudhui yake ilikuwa ni Akili Mnemba (AI) huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, chini ya kaulimbiu "Kutumia AI kwa Ustawi na Ushirikiano wa Afrika."

Akibainisha kuwa bara la Afrika linaingia kwenye zama za mabadiliko katika mwelekeo wake wa maendeleo, Waziri Mkuu Abiy amesema matumizi mazuri ya Akili Mnemba nyumbani yanaweza kutumika kama kichocheo cha ustawi jumuishi na kuingiza kasi kubwa katika mafanikio ya mpango wa maendeleo wa bara la Afrika wa miaka 50 yaani Ajenda ya 2063.

"Leo hii, tumesimama kwenye ukingo wa enzi mpya ambayo ina ahadi ya ustawi jumuishi kwa bara letu. Ni enzi inayoendeshwa na ubunifu wa nyumbani kwa kuktumia Akili Mnemba (Artificial Intelligence), na ina uwezo wa kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063," amesema Abiy Ahmed.

Vilevile amesisitizia haja ya bara la Afrika kubuni Akili Mnemba yake kwa sura, utamaduni na masharti yake yenyewe, akisema kuwa, Ethiopia inawekeza katika miundombinu ya kidijitali inayohusiana na AI na ukuzaji wa ujuzi kama ambayo inafanya kazi pia ya kutafsiri maono yake yaweze kuwa matokeo yanayoonekana.