Rais al Sisi atetea kuongezwa bajeti ya jeshi Misri
Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri ametetea kuongezwa bajeti ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo.
Akihutubia katika maadhimisho ya mwaka wa kwanza tangu kupanuliwa mfereji wa Suez, Rais wa Misri amesema kuwa katika hali ngumu iliyopo sasa, jeshi la Misri linapasa kuwa na nguvu na bajeti kubwa. Wachambuzi wa mambo wameitathmini hatua ya Rais Abdel Fattah kuwa inatokana na woga alionao kuhusu uwezekano wa kufanyika mapinduzi dhidi ya serikali yake hasa baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa hivi karibuni nchini Uturuki.
Duru za habari nchini Misri zimearifu kuwa, Rais al Sisi ametoa dikrii nambari 63 ya mwaka 2016 akitaka kufanyiwa marekebisho baadhi ya vipengee vya sheria za kustaafu kazi, bima na mafao wanayopasa kulipwa wanajeshi. Rais wa Misri ametoa dikrii hiyo baada ya wabunge wengi wa nchi hiyo wanaomuunga mkono kiongozi huyo kuafiki suala hilo.