Al-Burhan asisitiza kutoshirikishwa RSF katika mustakabali wa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129486-al_burhan_asisitiza_kutoshirikishwa_rsf_katika_mustakabali_wa_sudan
 Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan, amesisitiza kuwa, Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) hakitakuwa na nafasi katika mustakabali wa nchi hiyo.
(last modified 2025-11-16T06:33:27+00:00 )
Aug 13, 2025 11:00 UTC
  • Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan.
    Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan.

 Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan, amesisitiza kuwa, Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) hakitakuwa na nafasi katika mustakabali wa nchi hiyo.

Jenerali al-Burahn amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na mshauri wa Rais wa Marekani nchini Uswizi.

Kanali ya al-Jazeera ya Qatar imeripoti, ikinukuu vyanzo, kwamba Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan, alikutana na Massad Boulos, mshauri wa Rais Trump katika masuala ya Afrika, nchini Uswizi. Kulingana na chanzo hicho, al-Burhan alielezea upinzani wake dhidi ya kushirikishwa "Kikosi cha Usaidizi wa Haraka RSF) katika mustakabali wa Sudan. Jenerali Al-Burhan amesisitiza kuwa, hakubaliani na pendekezo lolote la kutaka kushirikishwa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) katika uongozi wa Sudan.

Nchi ya Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya wiki kadhaa za mvutano juu ya mpango wa kuunganisha kikosi cha RSF katika jeshi na kutokubaliana juu ya jedwali la uhamishaji wa mamlaka kwa utawala wa kiraia na uongozi wa kikosi kimoja.

Jenerali Hamdan Dagalo, Kiongozi wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) 

 

Mapigano hayo yaliongezeka mara ya kwanza katika mji mkuu, Khartoum, na maeneo muhimu kama vile Darfur, na kuenea haraka katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Usaidizi wa Haraka kinachoongozwa na Jenerali Hamdan Dagalo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka miwili sasa ambapo takriban raia 20,000 wamepoteza maisha na milioni 14 wamelazimika kuyahama makazi yao. Mashirika mbalimbali ya utoaji misaada yamekuwa yakitoa tahadhari kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Sudan.