Zakzaky: Mipango ya kuwafukuza Wapalestina Gaza, kuipokonya silaha Hizbullah itafeli
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Yaqoub Zakzaky amebainisha kuwa, mipango ya utawala wa Kizayuni ya kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza katika ardhi yao na kuipokonya silaha Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon kwa kutumia serikali ya Beirut itagonga mwamba.
Sheikh Zakzaky amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press mjini Abuja na kuongeza kuwa, Muqawama umejengeka katika msingi wa kusimama kidete, kumtegemea Allah na kufungamana na njia ya mapambano dhidi ya uchokozi wa pamoja wa Israel na Marekani.
Ameeleza bayana kuwa, "Utawala wa Kizayuni unapanga kuwaangamiza watu wa Gaza, haujali ikiwa hiyo itamaanisha kuua kila mtu. Baada ya miaka miwili ya mauaji ya halaiki kwa kutumia mabomu na njaa, sasa wanataka watu wafurushwe kwa nguvu ili kuiba rasilimali za Gaza, hasa gesi yake. Lakini hii itafeli. Wapalestina hawataiacha ardhi yao, kutoka mtoni hadi baharini."
Kiongozi huyo wa kidini na kijamii nchini Nigeria amebainisha kuwa, "Wazayuni wanadhani kuwapokonya silaha Hizbullah kutawadhoofisha, lakini nguvu yao halisi ni imani kwa Mwenyezi Mungu. Lebanon haitakuwa Ukingo mwingine wa Magharibi - watu wanasimama na Hizbullah kama watetezi wao wa kweli."
Katika siku za hivi karibuni, utawala wa Kizayuni umetangaza mipango ya wanajeshi kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina hadi kusini mwa Gaza kwa na kuwaweka kwenye mahema, baada ya kushindwa kufanya hivyo katika mauaji yake ya kimbari ya miaka miwili kwa kutumia njaa na mashambulizi ya mabomu.
Wakati huo huo, serikali ya Lebanon inaitaka Harakati ya Muqawama ya Hizbullah kusalimisha silaha zake, hatua iliyoelezwa na Katibu Mkuu wa kundi hilo la mapambano, Sheikh Naim Qassem siku ya Ijumaa kama, "kukabidhi usalama wa Lebanon kwa Israel," na aliapa kutoweka chini silaha.