Zaidi ya visa 100,000 vya kipindupindu vimeripotiwa Sudan huku njaa ikishadidi
Zaidi ya maambukizi 100,000 ya kipindupindu yameripotiwa katika nchi ya Sudan iliyokumbwa na vita katika mwaka mmoja, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) ilisema Jumatatu.
"Sudan inakumbwa na janga kubwa zaidi la njaa duniani, huku kipindupindu kikiendelea kusambaa. Njaa imethibitishwa katika baadhi ya maeneo ya nchi," OCHA ilisema katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Marekani X.
"Hatuwezi kusimama kando, watu wa Sudan wanahitaji msaada," iliongeza taarifa hiyo, ikitaja mlipuko wa kipindupindu kuwa ndio "mkubwa zaidi" katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Sudan, watu wasiopungua 2,561 wamefariki dunia kutokana na kipindupindu tangu kuzuka kwa janga hili mnamo Agosti 2024.
Mgogoro wa kipindupindu unakuja wakati vita kali kati ya jeshi la taifa na waasi wa kundi la RSF ambao walianzisha uasi dhidi ya serikali Aprili 2023, vikiendelea. Hadi sasa vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kuwalazimisha wengine milioni 14, kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Serikali ya Sudan inasema waasi wa RSF wanapata himaya ya kigeni hasa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Hata hivyo UAE imekanusha tuhuma za kuunga mkono waasi hao.