Bwawa la Renaissance; tishio kwa amani au fursa ya maendeleo?
Bwawa la Renaissance au an-Nahdha, mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme barani Afrika, ulizinduliwa rasmi na serikali ya Ethiopia siku ya Jumanne.
Abi Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia, alifungua rasmi Bwawa la Renaissance baada ya miaka 14 tangu kuanza ujenzi wake. Huku Ethiopia ikifungua bwawa hilo, Misri imetuma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiitaja hatua ya Ethiopia kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kusema kuwa Bwawa la an-Nahdha halitakuwa na uwajibikaji wowote wa kisheria au kisiasa kwa Misri na Sudan.
Bwawa la Renaissance, linalojulikana kama "Bwawa Kuu la Renaissance la Ethiopia", lilijengwa kwa ajili ya kuzalisha nishati kwa Ethiopia na nchi jirani. Katika kutetea mradi huu, viongozi wa Ethiopia wanaamini kuwa bwawa hilo sio tu litatoa umeme unaohitajika kwa mamilioni ya watu wa nchi hiyo, bali pia litaruhusu Ethiopia kusafirisha umeme wa ziada kwa nchi jirani. Abi Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia, ameendelea kutaja bwawa hili kama fursa ya pamoja ya maendeleo na kusisitiza kuwa mradi huu sio tishio kwa nchi zilizo chini ya Mto Nile.
Lakini pamoja na taarifa zote za viongozi wa Ethiopia, Misri ina wasiwasi sana kuhusu kufunguliwa kwa bwawa hilo. Nchi hiyo ambayo hudhamini maji yake yote safi kutoka Mto Nile, imetangaza upinzani wake kwa mradi huu tangu miaka mingi iliyopita. Sasa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesisitiza kuwa mradi huu ni ukiukaji wa mikataba ya kihistoria ambayo imetiwa saini kuhusu kugawana maji ya Mto Nile. Misri inaichukulia hatua hiyo ya Ethiopia kama ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za nchi zilizo chini ya Mto Nile na kusisitiza kuwa matokeo yoyote ya mradi huu ni batili na hayaihusu Misri.
Kwa mtazamo wa Cairo, upunguaji wowote wa mtiririko wa maji ya Nile unaweza kuwa na matokeo mabaya kwa kilimo, usambazaji maji ya kunywa na utulivu wa kijamii. Misri imesisitiza mara kwa mara kwamba Mto Nile sio tu ni chanzo cha asili cha maji, bali pia ni sehemu ya utambulisho wa kihistoria na ustaarabu wa nchi. Viongozi wa Cairo, akiwemo Rais Abdel Fattah al-Sisi, wameonya kwamba usalama wa maji ya Misri ni "mstari mwekundu" kwao na kwamba ikiwa watatishiwa, watachukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Katika miaka ya hivi karibuni, Misri imejaribu kutumia diplomasia ya pande kadhaa, ikiwa ni pamoja na upatanishi wa Marekani, Umoja wa Afrika, Russia na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, kufikia makubaliano kuhusu namna ya kujaza maji na kuendesha bwawa hilo, lakini juhudi hizo hadi sasa hazijafanikiwa.

Misri, ambayo idadi ya watu wake imeongezeka kwa kasi na kufikia zaidi ya watu milioni 100, inategemea Mto Nile kwa kusambaza zaidi ya asilimia 90 ya maji yake. Abbas Sharaki, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Cairo, anasema katika muktadha huu kwamba takriban asilimia 93 ya Misri ni jangwa ambapo hakuna watu wanaoishi kwenye jangwa hilo. Watu milioni 107, wanaishi kando kando ya Mto Nile na ustaarabu wa nchi hiyo umejengwa kwenye mto huo. Mto Nile ni maisha ya Wamisri. Mhadhiri huyo anaonya kuwa bwawa hilo litahifadhi mita za ujazo bilioni 64 za maji ambayo kwa kawaida hutiririka kuelekea Misri. Hii ni hasara kubwa kwa Misri.
Sudan pia ina nafasi maalum katika mlingano huu. Kwa upande mmoja, nchi hii ina wasiwasi kuhusu taathira hatari za kimazingira zinazoweza kutokea kutokana na usimamizi mbaya wa mabwawa, hasa katika hali ya kutokea mafuriko yanayoweza kuathiri usalama wa mabwawa yaliyoko chini ya mto huo. Katika upande wa pili, Sudan inaweza kunufaika na umeme wa bei nafuu na udhibiti bora wa rasilimali za maji, hasa katika maeneo ya mpakani na Ethiopia. Kwa hiyo, msimamo wa Sudan umeyumbayumba katika miaka ya hivi karibuni ambapo wakati mwingine imekuwa ikiunga mkono Misri na wakati mwingine Ethiopia, lakini kwa sasa inapinga mradi wa bwaha hilo.
Kwa kufunguliwa rasmi Bwawa la an- Nahdha siku ya Jumanne, Ethiopia imeongeza kiwango cha mivutano katika eneo huku makubaliano ya pande zote na ya lazima kutekelewa kati ya Ethiopia, Misri na Sudan yakiwa bado hayajafikiwa. Kuhusu suala hili, inaonekana kwamba suluhisho la mgogoro huu mgumu linaweza kupatikana tu kwa njia ya diplomasia amilifu na ushirikiano wa kikanda. Ni wazi kuwa uingiliaji wowote wa kigeni na ukosefu wa uratibu kati ya nchi husika, hasa katika uwanja wa usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji, sio tu unaweza kuwa tishio kwa utulivu wa kikanda, bali pia utafanya kuwa vigumu zaidi kufikiwa makubaliano thabiti yanayokubalika kwa nchi hizo zote.