Rais wa Afrika Kusini ataka kushughulikiwa changamoto za kiuchumi duniani
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametoa mwito kwa taasisi za kimataifa kufanya mageuzi ya maana ambayo yatashughulikia changamoto zinazoukabili uchumi wa dunia.
Amesema: "Wakati uchumi wa dunia umeonyesha uthabiti kwa kiasi fulani, lazima tukubali kwamba ukuaji wake ni mdogo na madeni ni makubwa. Hali hiyo inatokana na ufadhili mdogo wa kifedha. Tunahitaji mageuzi ya maana ya matumizi ya fedha kimataifa."
Rais wa Afrika Kusini amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje ambao ulifanyika wakati mmoja na Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York, Marekani.
Rais Ramaphosa aliwakumbusha viongozi wa dunia kwamba kuna wajibu wa kushughulia mpango wa kuondoa pengo la ufadhili wa maendeleo endelevu na kuundwa upya mfumo wa fedha wa kimataifa.
Afrika Kusini hivi karibuni ilizindua Kamati ya G20 ya Wataalamu Wanaojitegemea ili kukabiliana na ukosefu wa usawa na ugawaji mbovu wa utajiri ulimwenguni.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais Ramaphosa amesema: "Zaidi ya asilimia 85 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa sasa hayako sawa, huku kukiwa na vikwazo vikubwa katika kupambana na njaa, umaskini uliokithiri na kuongezeka ukosefu wa usawa."
Pia amesema: "Matukio mabaya ya hali ya hewa yanaleta hasara kubwa, hasa katika maeneo yote ya Afrika na maeneo mengine yenye mazingira magumu ya hali ya hewa. Vita na migogoro vinasababisha hasara kubwa ya maisha ya raia, mamilioni ya watu wanalazimika kuyahama makazi yao na kusababisha majanga ya kibinadamu."