Rais wa Madagascar alaani uporaji, atoa mwito wa utulivu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131306-rais_wa_madagascar_alaani_uporaji_atoa_mwito_wa_utulivu
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amelaani matukio ya vurugu yaliyotokea hasa katika mji mkuu Antananarivo na kuwataka wananchi wote wa Madagascar kuwa watulivu.
(last modified 2025-09-27T06:53:06+00:00 )
Sep 27, 2025 06:53 UTC
  • Rais wa Madagascar alaani uporaji, atoa mwito wa utulivu

Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amelaani matukio ya vurugu yaliyotokea hasa katika mji mkuu Antananarivo na kuwataka wananchi wote wa Madagascar kuwa watulivu.

Amesema: Ninalaani vitendo vya uharibifu vilivyopelekea kushuhudiwa matukio ya uporaji na uharibifu wa mali na biashara. Ninalaani vitendo hivyo na nia chafu ya kupandikiza chuki na  uharibifu katika nchi yetu.

Maandamano yaliandaliwa siku ya Alkhamisi huko Antananarivo kupinga kukatika umeme mara kwa mara na uhaba wa maji. Maandamano hayo yalishadidi polepole mpaka kutokea uporaji katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo ambayo ni kisiwa kikubwa zaidi kwenye Bahari ya Hindi.

Alkhamisi usiku, Angelo Ravelonarivo, gavana wa Antananarivo, alitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa moja kamili usiku hadi saa 11 alfajiri  katika mji mkuu na maeneo yake ya karibu hadi hali ya utulivu itakaporejea.

Rajoelina, ametoa mwito huo akiwa New York, Marekani, kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na amesema: "Mgawanyiko na chuki si suluhisho. Makabiliano yanasababisha uharibifu tu na hakuna anayefaidika nayo isipokuwa wale wanaotafuta maslahi yao binafsi."

Ikumbukwe pia kwamba jana Ijumaa, Rais wa Madagascar alimfuta kazi waziri wake wa nishati katika jitihada za kutuliza maandamano yaliyotokana na kulalamikia kukatwa umeme mara kwa mara na uhaba wa maji. Polisi walitumia risasi za mpira na gesi ya kutoa machozi kutawanya umati wa watu, wengi wao wakiwa ni vijana wa mji mkuu Antananarivo siku ya Alhamisi.

Waandaaji wa maandamano hayo waliwataka watu wasiofurahishwa na serikali ya Rajoelina kumiminika kwa wingi mitaani kufanya maandamano ya amani mpaka leo Jumamosi na kujiepusha na matukio ya uporaji na uharibifu wa mali yaliyotokea juzi Alkhamisi.