Sudan yatoa "tahadhari nyekundu" kuhusu uwezekano wa kutokea mafuriko nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131402-sudan_yatoa_tahadhari_nyekundu_kuhusu_uwezekano_wa_kutokea_mafuriko_nchini
Sudan imetoa "tahadhari nyekundu" kuhusu uwezekano wa kutokea mafuriko katika majimbo matano kando ya Mto Nile, ikisema kuwa viwango vya maji vimeongezeka katika vijito vyake viwili vikuu, Blue na White Nile.
(last modified 2025-11-05T05:46:17+00:00 )
Sep 30, 2025 02:29 UTC
  • Sudan yatoa

Sudan imetoa "tahadhari nyekundu" kuhusu uwezekano wa kutokea mafuriko katika majimbo matano kando ya Mto Nile, ikisema kuwa viwango vya maji vimeongezeka katika vijito vyake viwili vikuu, Blue na White Nile.

Wizara ya Umwagiliaji ya Sudan imewataka wakazi wa majimbo ya Khartoum, River Nile, White Nile, Sennar na Blue Nile kuchukua hatua za tahadhari kwa sababu mafuriko yanaweza kuathiri ardhi ya kilimo na makazi ya watu.

Baadhi ya wakulima katika jimbo la River Nile wamelazimika kuuza haraka zao lao la vitunguu kufuatia kuripotiwa mafuriko katika maeneo ya mabondeni ambayo yangeathiri kilimo. 

Siku ya Jumapili Wizara ya Umwagiliaji ya Sudan ilitahadharisha kuwa mtiririko wa maji umekuwa mkubwa kwa siku nne mfululizo huku mabwawa katika jimbo la River Nile yakimwaga maji ya ziada. 

Mapema mwezi huu, mamlaka husika za Sudan zilieleza kuwa zaidi ya familia 21,000 zimeathirika na mafuriko na mvua kubwa katika majimbo 11 nchini humo tangu mwezi Juni mwaka huu.