Raia 70,000 wa Sudan Kusini wakimbilia Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13168-raia_70_000_wa_sudan_kusini_wakimbilia_uganda
Idadi ya wananchi wa Sudan Kusini waliokimbilia nchini Uganda imepindukia watu 70,000.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 13, 2016 03:25 UTC
  • Raia 70,000 wa Sudan Kusini wakimbilia Uganda

Idadi ya wananchi wa Sudan Kusini waliokimbilia nchini Uganda imepindukia watu 70,000.

Aghalabu ya raia hao wa Sudan Kusini wameingia Uganda kupitia eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Baadhi ya raia hao wa Sudan Kusini waliohojiwa na mashirika ya habari wamesema baadhi ya wanaokimbia mapigano Sudan Kusini wamefia njiani huku wakiuawa na makundi ya wabeba silaha baada ya kuwasili Uganda. Hivi karibuni raia watatu wa Sudan Kusini waliuawa na kundi la wabeba silaha katika mji wa Elegu, kaskazini mwa Uganda.

Wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Uganda

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, maelfu ya raia wa Sudan Kusini wamekimbilia katika nchi jirani ya Uganda.

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR akthari ya raia hao wa Sudan Kusini wanaoingia nchini Uganda wanataabika na tatizo la njaa na lishe duni.

Mapigano kati ya askari wa mahasimu wawili wa kisiasa nchini Sudan Kusini yalianza mapema Julai

Kuanzia Julai 7 mwezi uliopita mji mkuu Juba ulianza kushuhudia mapigano ya umwagaji damu baina ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomtii Riek Machar ambaye ni Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo. Hadi sasa watu wasiopungua 300 wameripotiwa kuuawa katika mapigano hayo.