Tshisekedi amtaka Kagame aache kuwaunga mkono waasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131808-tshisekedi_amtaka_kagame_aache_kuwaunga_mkono_waasi
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amemtaka mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kuacha kuwasaidia waasi mashariki ya DRC na kutengeneza amani.
(last modified 2025-10-10T02:31:12+00:00 )
Oct 10, 2025 02:31 UTC
  • Tshisekedi amtaka Kagame aache kuwaunga mkono waasi

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amemtaka mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kuacha kuwasaidia waasi mashariki ya DRC na kutengeneza amani.

Rais Tshisekedi amesema hayo katika mkutano wa Global Gateway Forum mjini Brussel Ubelgiji ambao rais Kagame pia anahudhuria.

Tshisekedi, alizungumza baada ya Kagame kuzungumza kwenye mkutano huo wa uwekezaji ulioandaliwa na Umoja wa Ulaya jijini Brussels.

“Natangaza kwenye mkutano huu na kwa dunia nzima kufikisha mkono wangu kwako rais ilitufanye amani.” Alisema Rais Tshisekedi.

"Wacha tuwe na ujasiri wa kujiangalia na kujiuliza tatizo liko wapo na kuchukua uamuzi unaostahili kwa ajili ya watu wetu” aliongeza Rais wa DRC.

Kagame hakuwa amezungumzia moja kwa moja mzozo wa mashariki ya DRC wakati alipopewa nafasi ya kuzunguza.

Alisikika tu akigusia hotuba ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye wakati akiongea alisema alihisi kupata nguvu ya kutegeneza amani baada ya kuwaona wenzake wa DRC na Rwanda.

Rais Kagame amewahi kunukuliwa akisema kuwa, mapigano yanayoendelea, yalianzishwa na waasi waliokuwa wamekimbilia nchini Uganda, sasa hii imegeuka vipi shida ya Rwanda?  Viongozi wa waasi hao na wapiganaji wake hawana ushirikiano na Rwanda, labda tunahusishwa kwa sababu wana asili ya Rwanda, wanazungumza Kinyarwanda na huenda ndio kosa lao nchini DRC na hii imesababisha mateso yao.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.