UNHCR yahimiza jamii ya kimataifa kuwasaidia wakimbizi wa Sudan nchini Chad
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132954-unhcr_yahimiza_jamii_ya_kimataifa_kuwasaidia_wakimbizi_wa_sudan_nchini_chad
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetoa mwito wa dharura wa kusaidiwa sana kimataifa maelfu ya watu waliokimbilia Chad kukwepa mauaji ya kimbari nchini Sudan. Wasudan wanaendelea kumiminika katika nchi jirani ya Chad kutoka eneo la Darfur la magharibi mwa Sidan.
(last modified 2025-11-09T02:39:33+00:00 )
Nov 09, 2025 02:39 UTC
  • UNHCR yahimiza jamii ya kimataifa kuwasaidia wakimbizi wa Sudan nchini Chad

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetoa mwito wa dharura wa kusaidiwa sana kimataifa maelfu ya watu waliokimbilia Chad kukwepa mauaji ya kimbari nchini Sudan. Wasudan wanaendelea kumiminika katika nchi jirani ya Chad kutoka eneo la Darfur la magharibi mwa Sidan.

Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR, Kelly Clements ametoa mwito huo baada ya kuwatembelea wakimbizi huko Farchana, Chad, ambao wamekimbilia nchini humo kutokea mji wa el-Fasher wa magharibi mwa Sudan.

Ameelezea kusikiliza hadithi za kutisha ambazo zimefufua kiwewe kwa familia za wananchi wa el-Fasher. Mji huo ulikuwa umezingirwa kwa siku 500 na kundi la waasi la RSF na baadaye kutekwa na waasi hao.

Kelly Clements amesema: Hawa ni watu wanaohitaji sana kusaidiwa. Wanahitaji kila kitu kuanzia mahali salama pa kukaa, mpaka maji safi, hadi uwezo wa kuanza upya maisha yao."

Clements aliishukuru Chad kwa kufungua mipaka yake na kutumika kama mwenyeji mkarimu wa wakimbizi kwa miongo kadhaa.

Vilevile amesisitiza kwamba nchi na mashirika ya misaada ya kibinadamu hayawezi kudhibiti mgogoro huo peke yake. "Wanahitaji msaada," amesema katika ujumbe wake wa moja kwa moja kwa jumuiya ya kimataifa.

Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR pia amesema kuwa: "Hapa ndipo tunapohitaji msaada endelevu wa jumuiya ya kimataifa ili kuweza kufanya mengi zaidi hapa Chad, lakini pia kujaribu kuzifikia jamii zenye mahitaji makubwa sana ndani ya Darfur."

Uingiaji wa watu nchini Chad ni matokeo ya moja kwa moja ya ghasia mbaya huko el-Fasher kufuatia mji huo kutekwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ambavyo vinashutumiwa vibaya kwa kufanya mauaji ya kutisha huko el-Fasher.