Afrika Kusini imejiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa G20 uliosusiwa na Marekani
Afrika Kusini inajiadaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa G20, unaowakutanisha viongozi kutoka mataifa tajiri duniani, kujadili masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumu na kisiasa. Maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika sikuu za Jumamosi na Jumapili ijayo yamekamilika.
Afrika Kusini inalenga kutumia mkutano huu kushinikiza mataifa tajiri, kuhakikisha kuwa mataifa yenye uchumi mkubwa yanatoa mikopo yenye masharti kwa mataifa yanayoendelea, lakini pia kuhakikisha kuwa, kuna usawa kwenye masuala mbalimbali ikiwemo vita vya mabadiliko ya tabianchi.
Rais wa Marekani ametangaza kuwa, hakuna maafisa wa Marekani watakaohudhuria mkutano wa kila mwaka wa Kundi la G20 huko Johannesburg, Afrika Kusini.
Matamshi haya, yanayotokana na madai yaliyokanushwa ya "mauaji ya halaiki ya wazungu" nchini Afrika Kusini, ni kifuniko tu cha nia halisi ya Trump ya kuiadhibu Afrika Kusini kwa kuishitaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa mauaji ya kimbari huko Gaza.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, kitisho cha Rais wa Marekani Donald Trump kwamba maafisa wa nchi yake hawatahudhuria mkutano wa G20 mjini Johannesburg ni hasara kwa Wamarekani.
"Tutafanya maamuzi ya kimsingi na kutokuwepo kwa Marekani ni hasara kwao," Ramaphosa alisisitiza. "Washington inakwepa jukumu muhimu sana inalopaswa kuchukua kama uchumi mkubwa zaidi duniani."
Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa, kutokuwepo kwa Marekani, kutatoa fursa kwa China, ambayo itawakilishwa na Waziri Mkuu Li Qiang, kutawala mazungumzo hayo na kushawishi uungwaji mkono wa sera zake.