Ethiopia yakanusha kuwepo kambi za waasi wa RSF katika ardhi yake
-
Ethiopia: Hakuna kambi za RSF hapa nchini
Ethiopia imekanusha madai ya kuwepo kambi za wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika ardhi yake, ikisema yanalenga kuibua ugomvi kati ya nchi hiyo na jirani yake, Sudan.
Afisa wa cheo cha juu wa serikali ya Ethiopia, ameiambia Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kwamba habari hizo hazina msingi, akisisitiza kwamba njia za mawasiliano zipo kati ya nchi hizo mbili katika ngazi mbalimbali.
Afisa huyo amesisitiza kwamba Ethiopia "haitaruhusu shughuli zozote za uadui dhidi ya nchi yoyote jirani," na kusema Addis Ababa inaheshimu umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Sudan.
Taarifa hiyo ya Ethiopia imetolewa baada ya vyanzo rasmi vya Sudan kuiambia Al Jazeera Net kwamba Khartoum inajiandaa kufungua uwanja mpya wa vita mashariki mwa nchi baada ya nchi jirani ya Ethiopia kuruhusu kuanzishwa kambi ya mafunzo kwa wapiganaji wa kundi la waasi la RSF na mamluki wa kigeni wanaoshirikiana nalo ili kushambulia jimbo la Blue Nile linalopakana na mipaka yake.
Vyanzo vya serikali ya Sudn ambavyo havikutaka kutajwa majina, vimeeleza kwamba serikali ya Ethiopia inafanya uratibu wa kijeshi na RSF kupitia mamlaka za kikanda zinazowaunga mkono, ambapo makubaliano yalifikiwa kuhusu njia za misaada, ujenzi wa kambi za mafunzo na kuandaa viwanja vya ndege.