Iran, China, Saudia zakutana kuimarisha uhusiano na kudumisha amani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i134128-iran_china_saudia_zakutana_kuimarisha_uhusiano_na_kudumisha_amani
Kikao cha tatu wa Kamati ya Pande Tatu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia na Jamhuri ya Watu wa China cha kufuatilia Makubaliano ya Beijing kilifanyika jana Jumanne hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na wajumbe wa ngazi za juu wa pande hizo tatu.
(last modified 2025-12-10T03:13:52+00:00 )
Dec 10, 2025 03:13 UTC
  • Iran, China, Saudia zakutana kuimarisha uhusiano na kudumisha amani

Kikao cha tatu wa Kamati ya Pande Tatu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudi Arabia na Jamhuri ya Watu wa China cha kufuatilia Makubaliano ya Beijing kilifanyika jana Jumanne hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na wajumbe wa ngazi za juu wa pande hizo tatu.

Kikao hicho kimefanyika kwa uenyekiti wa Majid Takht Ravanchi, Naibu wa Masuala ya Kisiasa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na kimehudhuriwa pia na ujumbe wa Saudi Arabia uliongozwa na Walid Al-Kharaji, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia na ujumbe wa China uliongozwa na Miao Deo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China.

Pande za Iran na Saudi Arabia zimetilia mkazo nia na azma yao ya kujitolea kutekeleza vifungu vyote vya Mkataba wa Beijing na kusaidia juhudi zinazoendelea za kuimarisha uhusiano na ujirani mwema kati ya nchi za eneo hili. Vilevile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia zimekaribisha jitihada chanya zinazoendelea kufanywa na Jamhuri ya Watu wa China katika kufuatilia utekelezaji wa Makubaliano ya Beijing.

Jamhuri ya Watu wa China imesisitiza kwamba itaendelea kuunga mkono na kuhimiza hatua zilizochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia za kuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri baina yao katika nyanja mbalimbali.

Nchi hizo tatu zimetoa mwito wa kusitishwa mara moja jinai na uchokozi wa Israel dhidi ya nchi za Palestina, Lebanon na Syria, na zimelaani jinai za Israel na Marekani za kuivamia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwezi Juni mwaka huu. Tehran pia imezishukuru Saudi Arabia na China kwa msimamo wao thabiti wa kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu wakati wa vita hivyo vya siku 12 vilivyoanzishwa na Israel na Marekani dhidi ya Iran.