Tinubu: Jeshi la Nigeria ‘lililinda’ Benin kufuatia jaribio la mapinduzi
Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, amesema vikosi vya ulinzi vya nchi yake vilisaidia kulinda taifa jirani la Benin baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi Jumapili.
Kupitia ujumbe alioweka katika mtandao wa X, Tinubu alieleza kuwa kwa amri yake, “jeshi la Nigeria limesimama kwa ujasiri kama mlinzi na mtetezi wa utaratibu wa kikatiba katika Jamhuri ya Benin, kwa mwaliko wa serikali.”
Rais wa Benin, Patrice Talon, akihutubia kupitia televisheni ya taifa, alisema hali imedhibitiwa kikamilifu na akawahakikishia wananchi kuwa wanaweza kuendelea na shughuli zao kwa utulivu kuanzia jioni hiyo.
Mapema Jumapili, kundi la wanajeshi waliojitambulisha kama “Kamati ya Kijeshi ya Ujenzi Upya” (CMR) liliteka televisheni ya taifa na kutangaza kuwa “Bwana Patrice Talon ameondolewa madarakani kama rais wa jamhuri.”
Tangazo hilo lilijibiwa haraka na mashambulizi ya kutoka kwa vikosi vya askari watiifu kwa Talon. Jaribio hilo lilisambaratishwa kabisa kufuatia mashambulizi ya anga kutoka Nigeria na kupelekwa kwa wanajeshi kutoka mataifa mengine ya ukanda huo. Vyanzo vya kijeshi na usalama vya Benin vilisema takribani wanajeshi kadhaa, wakiwemo waliopanga jaribio hilo, wamekamatwa.
Ukanda wa Afrika Magharibi umekumbwa na wimbi la mapinduzi katika miaka ya karibuni, ikiwemo majirani wa kaskazini mwa Benin, Niger na Burkina Faso pamoja na Mali, Guinea na hivi karibuni Guinea-Bissau.
Talon anatarajiwa kukabidhi madaraka Aprili mwakani baada ya miaka 10 ya uongozi ulioshuhudia ukuaji wa uchumi, ingawa serikali yake bado inapambana na changamoto za kiusalama kaskazini mwa nchi.
Wakati huohuo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS. imetangaza kuwa wanajeshi kutoka Ghana, Côte d’Ivoire, Nigeria na Sierra Leone wanapelekwa Benin “kuunga mkono Serikali na Jeshi la Jamhuri ya Benin kulinda utaratibu wa kikatiba.”