Ethiopia yawarejesha nyumbani zaidi ya raia 27,000 waliokwama nje ya nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135030-ethiopia_yawarejesha_nyumbani_zaidi_ya_raia_27_000_waliokwama_nje_ya_nchi
Serikali ya Ethiopia imetangaza kwamba imewarejesha nyumbani zaidi ya raia 27,300 waliokuwa wamekwama katika nchi za Myanmar na Saudi Arabia katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.
(last modified 2026-01-02T10:13:33+00:00 )
Jan 02, 2026 10:13 UTC
  •  Ethiopia yawarejesha nyumbani zaidi ya raia 27,000 waliokwama nje ya nchi

Serikali ya Ethiopia imetangaza kwamba imewarejesha nyumbani zaidi ya raia 27,300 waliokuwa wamekwama katika nchi za Myanmar na Saudi Arabia katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Akiwasilisha ripoti ya utendaji wa wizara hiyo mbele ya Bunge la Taifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Gedion Timothewos amesema kuwa, serikali ya nchi yake imewarejesha nyumbani raia 1,300 ambao "walikuwa katika hali ngumu sana" nchini Myanmar.

Raia hao wa Ethiopia walidanganywa na madalali haramu walioahidi kuwapatia ajira huko kusini-mashariki mwa Asia. Walipofika huko, walipelekwa kwenye kambi zisizoruhusiwa katika maeneo yanayopakana na Myanmar na Thailand, ambako hali zao zilikuwa mbaya sana.

Waziri Timothewos pia amesema kuwa, kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia za serikali ya Ethiopia za kuwajali raia wake, nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika imewarejesha nyumbani zaidi ya raia 26,000 waliokwama nchini Saudi Arabia katika kipindi hicho cha miezi mitano iliyopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia amesisitiza pia kwamba juhudi kubwa za kuwarudisha nyumbani zinaonesha "ahadi kubwa ya serikali ya Ethiopia ya kuhakikisha kwamba haki na utu wa raia wake unalindwa ndani na nje ya nchi."

Serikali ya Ethiopia imewaonya wananchi wake kuendelea kuwa macho mbele ya "propaganda za udanganyifu" za wafanya magendo ya binadamu na kuepuka kutafuta fursa za ajira haramu nje ya nchi, hasa katika nchi ambazo hazina mikataba ya ajira na Ethiopia.