Dunia yampongeza Rais wa Zambia licha ya uchaguzi tata
Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa shakhsia na viongozi wa kwanza wa dunia kumpongeza Edgar Lungu kwa kushinda uchaguzi wa rais uliogubikwa na utata na ambao upinzani umeelekea mahakamani kupinga matokeo yake.
Katika ujumbe wake wa pongezi, Ban amewataka viongozi na kambi zote za kisiasa kuwa watulivu na kuhakikisha kuwa machafuko ya baada ya uchaguzi hayashuhudiwi nchini humo.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Koffi Annan, Rais wa Mawali Peter Mutharika na mwenzake wa Botswana Ian Khama pamoja na rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter kadhalika wamempongeza Rais Lungu kwa kuhifadhi kiti hicho katika uchaguzi wa Agosti 11.
Aidha waangalizi wa Umoja wa Ulaya na serikali ya Washington licha ya kukiri kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro za hapa na pale, lakini wamemtumia Rais Edgar Lungu ujumbe wa kumpongeza.
Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ) ilimtangaza Edgar Chagwa Lungu kuwa rais mteule kwa kupata asilimia 50.35 ya kura dhidi ya mpinzani wake Hakainde Hichelema aliyepata asilimia 47.63 ya kura.
Hata hivyo kiongozi wa chama cha upinzani cha UPND Hakainde Hichilema amesema kutangazwa mshindi Rais Edgar Lungu ni sawa na mapinduzi ya kijeshi dhidi ya mchakato wa kidemokrasia nchini Zambia na kwamba chama chake kitawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Katiba kupinga matokeo hayo akisisitiza kuwa, matakwa ya wananchi yamechakachuliwa na demokrasia kupuuzwa.