Uingereza yashirikiana na Imarati kumiliki bandari ya Somaliland dhidi ya Sudan
-
Uingereza yashirikiana na Imarati kumiliki bandari ya Somaliland dhidi ya Sudan
Serikali ya Uingereza imeripotiwa kumiliki bandari ya kimkakati inayodhibitiwa na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika eneo la Somaliland lililotangaza kujitenga la Somalia. Bandani hiyo ni sehemu ya mtandao wa miundombinu ya Imarati inayotumika kuvipelekea silaha Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyofanya mauaji ya umati nchini Sudan.
Hayo yametangazwa na televisheni ya Press TV na kuongeza kuwa, katika hali ambayo, ushirikiano wa Uingereza na DP World katika bandari ya Berbera unaonekana kuzusha maswali mengi kuhusu mgongano wa maslahi kati ya shughuli zake za kibiashara na madai yake ya kutumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro unaoendelea nchini Sudan.
Uingereza, kama Marekani na Umoja wa Ulaya, imewawekea vikwazo makamanda wa RSF wanaotuhumiwa kufanya ukatili ikiwa ni pamoja na mauaji ya umati, ukatili wa kingono na mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia huko El Fasher, Sudan.
Licha ya Imarati kuendelea kukanusha kulipa silaha kundi la RSF linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo - anayejulikana zaidi kama Hemedti, lakini ushahidi uliopo, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa safari za ndege, orodha ya mizigo na vyanzo vingi rasmi nchini Sudan na kwingineko, unaonesha kwamba nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi ndiyo inayohusika zaidi katika vita vya Sudan kupitia kuwasaidia waasi wa RSF.
Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, Abu Dhabi imetumia kile ambacho rais wa Marekani Donald Trump amekiita "fedha zake zisizo na kikomo" kuishinikiza London kutotaja kuhusika kwake katika mgogoro wa Sudan.
Vifaa vya kijeshi vilivyotengenezwa Uingereza na kupelekewa RSF kupitia Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) vimegunduliwa nchini Sudan mara nyingi tu, na uhusiano mkubwa wa kibiashara wa Uingereza na Imarati unazidi kuhusishwa na kuchochea moto wa mapigano nchini Sudan.
Wataalamu wanasisitiza kwamba bandari ya Berbera ni sehemu ya msururu wa miundombinu inayomilikiwa na Muungano waa Falme za Kiarabu ambayo imeenea katika kona zote za Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu.