Matumaini baada ya DRC kupokea dozi 70,000 za chanjo ya Ebola
-
Wafanyakazi wa sekta ya afya katika mstari wa mbele kukabiliana na Ebola
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Africa CDC, zimekaribisha uamuzi wa kuipatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, dozi 70,000 za chanjo ya Ervebo ili kuimarisha mapambano dhidi ya mlipuko wa Ebola aina ya Bundibugyo.
Taarifa iliyotolewa na WHO kanda ya Afrika imebainisha kuwa Kati ya hizo, dozi 50,000 zitatolewa kwa wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine walio mstari wa mbele, huku dozi 20,000 zikitumika katika majaribio ya kitabibu kubaini ikiwa chanjo hiyo inaweza kuwalinda binadamu dhidi ya virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.
Kwa sasa, chanjo ya Ervebo imeidhinishwa kutumika dhidi ya Ebola aina ya Zaire. Ingawa tafiti za awali kwenye maabara na wanyama zinaonesha kuwa huenda ikatoa kinga dhidi ya aina ya Bundibugyo, ufanisi wake kwa binadamu bado haujathibitishwa.
Wakati huo huo serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imezindua mpango wa dharura wa kuzuia kuenea kwa Ebola kando ya Mto Kongo
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Alhamisi ilizindua mpango wa dharura wa kuimarisha ufuatiliaji na maandalizi dhidi ya Ebola kando ya Mto Kongo, huku mamlaka zikilenga kuzuia ukanda mkuu wa usafirishaji wa mto huo usigeuke kuwa njia ya kueneza ugonjwa huo katika maeneo mapana zaidi.
Mpango huo uliopewa jina la “Mto Kongo Bila Ebola” unalenga kuzuia mlipuko wa Ebola kusambaa kuelekea miji mikubwa iliyoko kando ya mto huo, hususan Mbandaka na mji mkuu Kinshasa. Aidha, unalenga kupunguza hatari ya maambukizi kuvuka mipaka na kufika katika nchi jirani, zikiwemo Jamhuri ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
DRC ilitangaza mlipuko huu wa sasa wa Ebola tarehe 15 Mei. Tangu wakati huo, mlipuko huo umeua watu wasiopungua 2300, na hivyo umegeuka kuwa janga kubwa zaidi na hatari zaidi la Ebola kuwahi kurekodiwa nchini humo, na pia ni la pili kwa ukubwa duniani kote.