Ethiopia yaanza ujenzi wa 'uwanja mkubwa zaidi wa ndege barani Afrika'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135354-ethiopia_yaanza_ujenzi_wa_'uwanja_mkubwa_zaidi_wa_ndege_barani_afrika'
Ethiopia imezindua ujenzi wa 'uwanja mkubwa zaidi wa ndege barani Afrika' utakaogharimu dola bilioni 12.5 za Marekani.
(last modified 2026-01-11T06:33:34+00:00 )
Jan 11, 2026 06:33 UTC
  • Ethiopia yaanza ujenzi wa 'uwanja mkubwa zaidi wa ndege barani Afrika'

Ethiopia imezindua ujenzi wa 'uwanja mkubwa zaidi wa ndege barani Afrika' utakaogharimu dola bilioni 12.5 za Marekani.

Shirika la habari la Reuters limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, Shirika la Ndege la Ethiopia jana Jumamosi lilianza rasmi ujenzi wa mradi huo ambao maafisa wa Addis Ababa wanasema utakuwa uwanja mkubwa zaidi wa ndege barani Afrika, utakapokamilika mwaka 2030.

Shirika hilo la ndege linalomilikiwa na serikali lilipewa kandarasi ya kutengeneza uwanja huo wa ndege wenye njia nne, katika mji wa Bishoftu, ulioko yapata kilomita 45 (maili 28) kusini mashariki mwa Addis Ababa.

"Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bishoftu utakuwa mradi mkubwa zaidi wa miundombinu ya anga katika historia ya Afrika," Waziri Mkuu Abiy Ahmed Ali amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X. Uwanja huo utakuwa na nafasi ya kuegesha ndege 270 na uwezo wa kubeba abiria milioni 110 kwa mwaka.

"Hiyo ni zaidi ya mara nne ya uwezo wa uwanja mkuu wa ndege wa sasa wa Ethiopia, ambao utafikia kikomo chake cha uwezo wa mapokezi katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo," Abiy amesema.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miundombinu na Mipango wa shirika hilo la ndege, Abraham Tesfaye amewaambia waandishi wa habari kuwa, shirika hilo litafadhili asilimia 30 ya fedha za mradi huo, huku kiwango kilichosalia kikisimiwa na fedha za mikopo na wafadhili.

Tayari shirika hilo limetenga dola milioni 610 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi huo, ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja, huku wakandarasi wakuu wakitazamiwa kuanza kazi mwezi Agosti mwaka huu 2026.