Wanawake Zimbabwe wafanya maandamano ya kulalamikia serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13564-wanawake_zimbabwe_wafanya_maandamano_ya_kulalamikia_serikali
Sambamba na kupamba moto maandamano ya kupinga serikali ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika kila pembe ya Zimbabwe, maelfu ya wanawake wa nchi hiyo nao pia jana waliandamana katika mji wa Bulawayo wakitaka watoto wao wapatiwe elimu bila ya malipo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 19, 2016 03:37 UTC
  • Wanawake Zimbabwe wafanya maandamano ya kulalamikia serikali

Sambamba na kupamba moto maandamano ya kupinga serikali ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika kila pembe ya Zimbabwe, maelfu ya wanawake wa nchi hiyo nao pia jana waliandamana katika mji wa Bulawayo wakitaka watoto wao wapatiwe elimu bila ya malipo.

Maandamano hayo yaliyofanyika kwa kaulimbiu ya "Susia Ada ya Shule" yaliandaliwa na jumuiya iitwayo Wanawake wa Zimbabwe Inukeni (WOZA) ambayo imewasilisha ombi la malalamiko kwa waziri mhusika karibu na kuanza muhula mpya wa masomo mapema mwezi ujao.

Mratibu wa WOZA Jennie Williams alisema:"tunaitaka serikali iheshimu wajibu wake wa kikatiba wa kutoa elimu kwa wote."

Maandamano ya kulalamikia ajira Zimbabwe

Kwa mujbu wa jumuiya za wazazi, malefu ya watoto wamefukuzwa skuli sehemu mbalimbali nchini Zimbabwe kwa kushindwa kulipa ada ya masomo kwa wakati huku mamilioni ya Wazimbabwe wakiwa wanaishi bila ya kuwa na ajira. 

Jumuiya za wafanyakazi zinakadiria kuwa karibu asilimia 90 ya wananchi wote milioni 14 wa Zimbabwe hawana ajira.

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umeeleza katika ripoti yake ya karibuni kuwa uchunguzi wa kawaida unaofanya unaendelea kuonyesha kushuka kwa kiwango cha mahudhurio ya wanafunzi maskulini lakini haujaweza kupata idadi halisi ya wanafunzi hao katika madarasa.

Rais Robert Mugabe

Maandamano ya jana yaliyoshirikisha wanawake wapatao 2,000 yamefanyika huku mashinikizo dhidi ya Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 92 yakizidi kuongezeka kutokana na hali mbaya ya uchumi inayoendelea kushuhudiwa nchini humo.../