Jeshi la Mali: Makumi ya wanamgambo wameuawa karibu na Segou
Jeshi la Mali limetangaza habari ya kufanya wimbi la mashambulizi yaliyoratibiwa ambayo yamewaua makumi ya washukiwa wa ugaidi, wakati wa operesheni zilizofanyika magharibi mwa jiji la Segou, katikati ya nchi.
Jeshi hilo limesema operesheni hizo zilifuatia ufuatiliaji wa eneo uliofanywa mnamo Februari 7, ambapo kundi lenye silaha liliviziwa hadi eneo lenye misitu magharibi mwa Segou ambapo lilijaribu kujificha. Taarifa ya Mkuu wa Majeshi ya Mali imesema takriban wapiganaji 15 walishambuliwa na kuuawa katika shambulio la kwanza.
Shambulio la pili liliwaangamiza takriban wanamgambo 10 na vifaa vyao vya usafirishaji walipojaribu kuingia katika mtumbwi kwenye ukingo wa Mto Niger, magharibi mwa Segou.
Katika eneo hilo hilo, kundi jingine la wanamgambo wapatao 10 waliokuwa wakisafiri kwa pikipiki liligunduliwa na kuangamizwa. Mkuu wa Majeshi ya Mali amesema operesheni hizo zitaendelea nchini kote.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeshi la Mali lilitangaza kuwa limewaua zaidi ya magaidi 100 katika mashambulizi ya anga liliyofanya kwenye eneo la msitu katikati mwa nchi, na kuyataja mashambulio hayo kuwa ni operesheni muhimu dhidi ya magaidi katika eneo hilo.
Mali imekabiliwa na changamoto ya usalama tangu mwaka 2012, sambamba na kukumbwa na mashambulizi ya magaidi, hasa katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa nchi. Makundi hayo ya magaidi yameshtumiwa kwa kuzuia mafuta kuingia nchini humo katika miezi ya hivi karibuni.