Somalia: Israel kuitambua 'Somaliland' ni ukiukaji wa sheria za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136448-somalia_israel_kuitambua_'somaliland'_ni_ukiukaji_wa_sheria_za_kimataifa
Serikali ya Somalia imeendelea kukosoa vikali uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kutambua kama nchi eneo la Somalia lililojitenga na kujiita Somaliland, ikisema kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa sheria na misingi ya kimataifa, huku ikibainisha kuwa Tel Aviv ina historia ya kukiuka kanuni hizo kwa miaka mingi.
(last modified 2026-02-10T02:26:22+00:00 )
Feb 10, 2026 02:26 UTC
  • Waziri wa Haki na Masuala ya Katiba wa Somalia, Hassan Moallim Mohamud
    Waziri wa Haki na Masuala ya Katiba wa Somalia, Hassan Moallim Mohamud

Serikali ya Somalia imeendelea kukosoa vikali uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kutambua kama nchi eneo la Somalia lililojitenga na kujiita Somaliland, ikisema kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa sheria na misingi ya kimataifa, huku ikibainisha kuwa Tel Aviv ina historia ya kukiuka kanuni hizo kwa miaka mingi.

Waziri wa Haki na Masuala ya Katiba wa Somalia, Hassan Moallim Mohamud, akiwa safarini Uturuki amewaambia waandishi wa habari kwamba:“Hatua ya Israel kutambua 'Somaliland' ni ukiukaji washeria za kimataifa na kanuni zilizokubalika kimataifa na hatua hiyo inaonesha wazi dharau ya Israel dhidi ya sheria na misingi ya kimataifa.”

Mnamo Desemba 26 mwaka jana, Israel ilitangaza rasmi kuwa imeitambua Somaliland kama taifa huru na lenye mamlaka kamili, na hivyo kuwa nchi pekee duniani kuchukua hatua hiyo, hatua ambayo ilizua upinzani mkali barani Afrika na miongoni mwa nchi za Kiarabu.

Waziri huyo amesisitiza kuwa hatua za aina hiyo hazilengi Somalia pekee, akieleza kuwa Israel imekuwa ikikuka sheria za kimataifa mara kwa mara.

Katika upande mwingine, Rais wa Somalia amelaani vikali kile hatua ya utawala wa Israel kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake, akiahidi “kukabiliana” na uwepo wowote wa kijeshi wa Israel katika eneo la Somalia la Somaliland ambalo limejitangazia uhuru.

Katika mahojiano siku ya Jumamosi, Hassan Sheikh Mohamud alisema hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru ni “kitendo cha kiholela, kilicho kinyume na misingi ya haki, na kisicho halali chini ya sheria za kimataifa.”

Somaliland ni eneo lililojitenga kaskazini-magharibi mwa Somalia, ambalo zamani lilikoloniwa na Uingereza. Licha ya tangazo la upande mmoja la kujitenga upande, eneo hilo bado linatambulika kimataifa kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Somalia.

Hatua ya Israel imefuatia ripoti kuwa utawala huo uliwasiliana na wahusika ndani ya Somaliland kujadili uwezekano wa kulitumia eneo hilo kwa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wakati wa vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza,vita ambavyo vimeua zaidi ya Wapalestina 72,000 na kuwaacha wengine zaidi ya 172,000 wakiwa wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.