Türk: Janga la haki za binadamu Sudan linaweza kuzuilika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136462-türk_janga_la_haki_za_binadamu_sudan_linaweza_kuzuilika
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba machafuko ya El Fasher, Sudan, ni “janga kubwa la haki za binadamu linaloweza kuzuilika,” kufuatia miezi ya kuzingirwa na njaa iliyochochewa na kundi la waasi la RSF. 
(last modified 2026-02-10T07:16:02+00:00 )
Feb 10, 2026 07:16 UTC
  • Türk: Janga la haki za binadamu Sudan linaweza kuzuilika

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ameliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba machafuko ya El Fasher, Sudan, ni “janga kubwa la haki za binadamu linaloweza kuzuilika,” kufuatia miezi ya kuzingirwa na njaa iliyochochewa na kundi la waasi la RSF. 

Akilihutubia baraza hilo mjini Geneva jana Jumatatu baada ya ziara yake nchini Sudan, Türk amesema maelfu ya raia waliuawa ndani ya siku chache tu mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya miezi 18 ya mashambulizi na kunyimwa mahitaji ya msingi. 

Amesema “Wajibu wetu wa pamoja ni kuwawajibisha waliohusika, na kuhakikisha hili halitokei tena.” 

Türk amesema ushuhuda uliokusanywa na ofisi yake unaonesha taswira ya kutisha ya uhalifu mkubwa uliotekelezwa wakati wa mashambulizi ya mwisho ya RSF. Wafanyakazi wake waliwahoji zaidi ya waathirika na mashahidi 140 nchini Sudan na mashariki mwa Chad, ambao wameripoti kwa yakini kuwa walishuhudia mauaji ya halaiki, mauaji ya kiholela na mashambulizi dhidi ya raia walipokuwa wakikimbia mji.

Türk amesema manusura wameelezea kuona miili ya watu ikiwa imetapakaa barabarani wakikimbia El Fasher, katika mandhari ambayo “mtu mmoja aliifananisha na siku ya hukumu.”

Türk amesema waasi wa RSF na waitifaki wao wametua unyanyasaji wa kijinsia umetumika “kwa utaratibu kama silaha ya vita."

Wakati wa ziara yake Sudan, Türk alikutana na manusura waliotoa ushuhuda wa ubakaji wa makundi na aina nyingine za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana.  Türk pia amethibitisha kuwa ofisi yake imebaini kusajiliwa na kutumiwa kwa watoto na kundi la RSF, ama kwa kulazimishwa au kwa kuwekwa chini ya shinikizo la kijamii.

Ameonya kuwa ukiukwaji kama huo unaweza kujirudia katika eneo la Kordofan, na akaitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka. 

Mapigano ya sasa Sudan yalianza Aprili 2023 wakati waasi wa RSF walipoanzisha vita dhidi ya serikali kuu ya Sudan kwa lengo la kunyakua madaraka. Makumi ya maelefu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni 12 kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya Sudan. Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu,  UAE, kuwa inawaunga mkono waasi hao wa RSF wanaotenda jinai.