Reuters: Kuna kambi ya siri ya wapiganaji wa RSF nchini Ethiopia
-
Kambi ya siri ya wapiganaji wa RSF nchini Ethiopia
Ripoti ya shirika la habari la Reuters, iliyotokana na picha za satalaiti na ushuhuda rasmi, imefichua kuwepo "kambi ya siri" nchini Ethiopia kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maelfu ya wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF), ambao wanapigana na jeshi nchini Sudan.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Reuters kuhusu picha za satalaiti na kebo ya kidiplomasia, kambi hiyo iko katika eneo la mbali la Benishangul-Gumuz nchini Ethiopia, kilomita 32 kutoka kwenye mpaka wa Sudan, na kilomita 101 kutoka Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance.
Vyanzo vinane, ikiwa ni pamoja na afisa mkuu wa serikali ya Ethiopia, vimeiambia Reuters kwamba mapema Januari eneo hilo lilipokea wapiganaji wapatao 4,300 kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi.
Picha za satalaiti zinaonyesha upanuzi mkubwa wa kambi hiyo katika eneo lenye misitu la wilaya ya Mingi katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mahema zaidi ya 640 na ujenzi wa kituo cha kudhibiti ndege zisizo na rubani katika uwanja wa ndege wa karibu wa "Asosa".
Taarifa ya kidiplomasia ya mwezi Novemba mwaka jana, iliitaja kambi hiyo kuwa na uwezo wa kubeba wapiganaji 10,000 na kuongeza kwamba, shughuli za kambi hiyo zilianza Oktoba baada ya kuwasili magari kadhaa ya Land Cruiser na malori makubwa.
Maafisa sita wameiambia Reuters kwamba wengi kati ya walioajiriwa katika kambi hiyo ni Waethiopia, lakini pia kuna raia wa Sudan Kusini na Sudan, wakiwemo baadhi wanachama wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini (SPLM-N), kundi la waasi la Sudan linalodhibiti baadhi ya maeneo ya jimbo jirani la Blue Nile.
Taarifa ua uchunguzi wa Reuters inasema, mkuu wa Kurugenzi ya Ujasusi ya Vikosi vya Ulinzi vya Ethiopia, Jenerali Getachew Gudina, ndiye anayesimamia kambi hiyo ya kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa kundi la waasi wa Sudan la RSF.
Picha hizo zimeonyesha kazi ya ujenzi katika uwanja wa ndege wa Assosa tangu Agosti 2025, ikiwa ni pamoja na jengo jipya la kuhifadhi ndege na maeneo ya lami ili kusaidia shughuli za ndege zisizo na rubani.
Wasemaji wa serikali ya Ethiopia na RSF wamekataa kutoa maoni kuhusu ripoti hiyo.
Tangu waasi wa RSF waanzishe vita dhidi ya serikali ya Sudan mwezi Aprili 2023, maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni 12 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi, huku mikoa kadhaa ikikumbwa na njaa na uhaba wa chakula.