Mawaziri Zimbabwe wapitisha muswada kumuwezesha Rais Mnangagwa kutawala hadi 2030
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136500-mawaziri_zimbabwe_wapitisha_muswada_kumuwezesha_rais_mnangagwa_kutawala_hadi_2030
Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limeunga mkono muswada unaokusudia kubadilisha katiba ili kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa kubakia madarakani hadi angalau mwaka 2030.
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Feb 11, 2026 07:03 UTC
  • Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe
    Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe

Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limeunga mkono muswada unaokusudia kubadilisha katiba ili kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa kubakia madarakani hadi angalau mwaka 2030.

Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, alitarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2028 baada ya kumaliza vipindi viwili vya miaka mitano. Lakini muswada huo unalenga kuongeza muda wa utawala wa rais kutoka miaka mitano hadi saba.

Mabadiliko mengine yanayopendekezwa ni pamoja na kuongeza muda wa wabunge kutoka miaka mitano hadi saba, kumruhusu rais kuchaguliwa na Bunge badala ya kupigiwa kura moja kwa moja na wananchi na kuongezwa idadi ya maseneta, ambapo rais ataweza kuteua maseneta 10 zaidi, jambo linaloongeza idadi ya viti vya Seneti hadi 90.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri jijini Harare siku ya Jumanne, Waziri wa Haki, Sheria na Masuala ya Bunge, Ziyambi Ziyambi, alisema muswada huo utapelekwa kwa Spika wa Bunge na kuchapishwa rasmi katika gazeti la serikali. Aliongeza kuwa baada ya uchapishaji, wananchi watapata kipindi cha siku 90 kushiriki mashauriano ya umma kabla ya muswada kuwasilishwa kwa majadiliano rasmi ya Bunge.

Waziri wa Habari, Uenezi na Utangazaji, Jenfan Muswere, alisema lengo la muswada ni kupunguza usumbufu unaohusiana na uchaguzi, kuhakikisha utulivu wa kisiasa, uendelevu wa sera, na ufanisi wa serikali.

Mnangagwa, anayejulikana kwa jina la “Mamba” kutokana na ujanja wake wa kisiasa, aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya mapinduzi ya kijeshi kumtoa Robert Mugabe. Alishinda uchaguzi wa rais mwaka 2018 na tena mwaka 2023, ingawa matokeo yalipingwa na wapinzani wake.

Rais Mnangagwa anaongoza chama cha ZANU-PF, ambacho kimekuwa madarakani tangu uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980, lakini hivi karibuni kimekabiliwa na mgogoro wa ndani kuhusu urithi wa uongozi.