Aug 21, 2016 03:58 UTC
  • Kongo yawatuhumu waasi sita kwa kuua raia

Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewatuhumu wanachama sita wa kundi la waasi wa Uganda kwa kushiriki katika mauaji wiki iliyopita, ambapo makumi ya raia waliuliwa mashariki mwa Kongo.

Kanali Jean-Paulin Esosa anayesimamia mahakama ya kijeshi ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini ameeleza kuwa waasi hao sita wanatuhumiwa kushiriki katika harakati za uasi na kutenda jinai dhidi ya binadamu, kufanya mauaji na ugaidi.

Waasi wa ADF-Nalu

Kanali Esosa ameongeza kuwa waasi hao sita ni pamoja na Waganda wawili, Mtanzania mmoja na Wakongo watatu. Waandishi habari waliohudhuria kikao cha wazi cha kusikiliza kesi inayowakabili watuhumiwa hao wamesema kuwa waasi hao sita wamekiri kuwa wamekuwa wakihudumu katika harakati ya Waasi wa Uganda wa ADF-Nalu, kundi linalobeba silaha kutoka Uganda ambalo limekuwepo huko Kongo kwa zaidi ya miongo miwili sasa. Itakumbukwa kuwa hivi karibuni waasi wa ADF-Nalu wamehusika katika mauaji ya umati ya raia wasiopungua 50 katika mji wa Beni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Raia wa Kongo wanailaumu serikali kwa kushindwa kuwalinda raia.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tags