Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia yapuuza madai ya kuwekewa sumu Lungu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136778-familia_ya_aliyekuwa_rais_wa_zambia_yapuuza_madai_ya_kuwekewa_sumu_lungu
Familia ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye alifariki dunia nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka jana na bado hajazikwa, imekanusha madai kwamba Lungu aliwekewa sumu.
(last modified 2026-02-19T02:22:27+00:00 )
Feb 19, 2026 02:22 UTC
  • Edgar Lungu
    Edgar Lungu

Familia ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye alifariki dunia nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka jana na bado hajazikwa, imekanusha madai kwamba Lungu aliwekewa sumu.

Polisi wa Afrika Kusini pia wanataka wapewe jukumu la utunzaji wa mwili wake kama sehemu ya uchunguzi wao, kulingana na familia ya mwanasiasa huyo aliyeaga dunia.

Katika barua kwa polisi, mawakili wanasema familia hiyo inashirikiana na "kesi za uhalifu", lakini wanasisitiza kwamba madai hayo "hayana msingi na hayana ushahidi wa kuaminika".

Ni mabadiliko ya hivi karibuni kuhusu hatima ya mwili wa Lungu, ambao bado upo katika chumba cha kuhifadhia maiti nchini Afrika Kusini, huku mgogoro wa kisheria ukioendelea kati ya familia yake na serikali ya Zambia kuhusu mahali anapopaswa kuzikwa.

Polisi nchini Afrika Kusini imekataa kutoa maoni yoyote kuhusu barua iliyotumwa na kampuni ya sheria ya Mashele Attorneys ya Johannesburg, ambayo inawakilisha familia ya Lungu.

Msemaji wa polisi, Brigedia Athlenda Mathe, amesema: "Hili ni jambo nyeti sana ambalo haliwezi kujadiliwa katika hatua hii."

Lungu alifariki dunia kutokana na ugonjwa ambao haujawekwa wazi akiwa na umri wa miaka 68 katika hospitali moja mjini Pretoria, Afrika Kusini. Alikuwa ameiongoza Zambia kuanzia 2015 hadi 2021, aliposhindwa katika uchaguzi kwa tofauti kubwa na Rais wa sasa, Hakainde Hichilema.

Serikali ya Zambia inataka mwili wa Lungu urudishwe nyumbani na afanyiwe mazishi ya kitaifa, kwa heshima kamili ya kitaifa, na mahakama ya Afrika Kusini ilitoa uamuzi ulioiunga mkono serikali mwezi Agosti mwaka jana.

Lakini wanafamilia ya Lungu wanataka mazishi ya faragha nchini Afrika Kusini kwani wanasema rais huyo wa zamani hakutaka Hichilema ahudhurie mazishi yake. Uhusiano kati ya wanasiasa hao wawili ulikumbwa na utata kwa muda mrefu.