Polisi Zimbabwe watumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13930-polisi_zimbabwe_watumia_mabomu_ya_kutoa_machozi_kutawanya_maandamano_ya_wapinzani
Askari polisi wa Zimbabwe wametumia mabomu ya kutoa machozi na mipira ya maji kuwatawanya vijana wa chama cha upinzani cha MDC waliokuwa wakiandamana kupinga ukatili unaofanywa na maafisa wa usalama
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 24, 2016 23:48 UTC
  • Polisi Zimbabwe watumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya maandamano ya wapinzani

Askari polisi wa Zimbabwe wametumia mabomu ya kutoa machozi na mipira ya maji kuwatawanya vijana wa chama cha upinzani cha MDC waliokuwa wakiandamana kupinga ukatili unaofanywa na maafisa wa usalama

Zaidi ya vijana 200 wafuasi wa chama cha upinzani cha Harakati kwa ajili ya Mabadiliko ya Kidemokrasia (MDC) waliandamana jana katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, siku mbili kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanywa na vyama vyote vya upinzani ili kujaribu kumlazimisha Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe azifanyie marekebisho sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2018.

Hata hivyo askari hao waliingilia kati maandamano hayo na kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji hao waliokuwa wakitaka kuwasilisha barua yao ya ombi kwenye ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani inayosimamia jeshi la Polisi.

Askari polisi wa Zimbabwe wakipambana na waandamanaji

Baadhi ya waandamanaji walijibu hujuma hizo za polisi kwa kuwarushia mitungi ya mabomu ya machozi na mawe polisi hao ambao waliwafukuza kwa mipira ya maji hadi nje ya ofisi kuu za chama cha MDC.

Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana la chama cha MDC Lovemore Chinopusta ameaviambia vyombo vya habari kuwa kumekuweko na hatua za makusudi za Polisi kujaribu kuwatisha, kuwanyanyasa na kuwaziba midomo wananchi wa Zimbabwe. 

Zimbabwe imekuwa na rekodi ya utumiaji nguvu na ukatili dhidi ya wapinzani wa Rais Mugabe, ambapo katika miezi michache iliyopita polisi ya nchi ilikandamiza maandamano ya kulalamikia ukosefu wa ajira, uhaba wa chakula na ufisadi serikalini.

Tsvangirai (kulia) na Mujuru (kushoto)

Kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai na aliyekuwa Makamu wa Rais Joice Mujuru wanatazamiwa kuongoza maandamano ya wapinzani ya siku ya Ijumaa.../