Polisi ya Zimbabwe yakabiliana tena na wapinzani wa serikali ya Mugabe
Kwa mara nyingine tena polisi nchini Zimbabwe imekabiliana na waandamanaji dhidi ya serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo, Harare.
Makabiliano hayo yamejiri leo Ijumaa wakati wapinzani walipoingia mitaani wakitaka kufanyika marekebisho katika mfumo wa uchaguzi nchini. Washiriki katika maandamano hayo wamemtaka Rais Robert Mugabe kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2018 sanjari na kuondoka kwake madarakani.
Waandamanaji pia wamemtuhumu Rais Mugabe kuwa anaongoza nchi hiyo kwa mfumo wa udikteta na wamemtaka aondoke mara moja madarakani.
Katika miezi ya hivi karibuni polisi ya nchi hiyo imekuwa ikikabiliana na maandamano ya kulalamikia ukosefu wa ajira na ufisadi nchini Zimbabwe, na inatumia nguvu kuzima malalamiko hayo ya wananchi.
Hivi karibuni pia askari polisi wa Zimbabwe walitumia mabomu ya kutoa machozi na mipira ya maji kuwatawanya vijana wa chama cha upinzani cha MDC waliokuwa wakiandamana kupinga ukatili unaofanywa na maafisa wa usalama.