Watu watatu wauawa katika machafuko Gabon, mamia watiwa mbaroni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14449-watu_watatu_wauawa_katika_machafuko_gabon_mamia_watiwa_mbaroni
Machafuko yameendelea kushuhudiwa katika mji mkuu wa Gabon Libreville baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais ambayo yamemrejesha tena madarakani Rais Ali Bongo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 02, 2016 00:00 UTC
  • Watu watatu wauawa katika machafuko Gabon, mamia watiwa mbaroni

Machafuko yameendelea kushuhudiwa katika mji mkuu wa Gabon Libreville baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais ambayo yamemrejesha tena madarakani Rais Ali Bongo.

Wapinzani wa Gabon ambao wameyakataa matokeo hayo wakisema mgombea wao Jean Ping ameporwa ushindi jana walimiminika katika mitaa na barabara za mji mkuu Libreville na kupelekea kuibuka mapigano kati yao na polisi. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, watu watatu wameshauawa katika vurugu baina ya waandamanaji na vikosi vya usalama vya kuzuia fujo.

Rais Ali Bongo aliyeshinda tena kiti cha Urais Gabon

Vikosi vya usalama nchini Gabon vimewakamata zaidi ya watu elfu moja katika siku ya pili ya ghasia zilizozushwa na wapinzani waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo Jumamosi iliyopita.

Rais Ali Bongo ambaye ndiye aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo amewalalamikia wafuasi wa upinzani ambao walimiminika mitaani siku ya Jumatano na kuchoma moto bunge la nchi hiyo. Amesema demokrasia haiwezi kupatikana kwa njia kama hizo.

Akizungumza na vyombo vya habari, Rais Bongo amesema ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi sio za kidemokrasia.

Wafuasi wa upinzani wameilalamikia serikali kwamba imefanya hila katika uchaguzi huo na kumtaka Rais Bongo kujiuzulu.

Vikosi vya usalama Gabon vikikabiliana na waandamanaji

Tume ya Uchaguzi ya Gabon ilitangaza kuwa, Rais Bongo ameshinda kiti cha urais kwa asilimia 49.80 akifuatiwa kwa karibu na mpinzani wake mkuu Jean Ping aliyewahi kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kutoka mwaka 2008 hadi 2012 ambaye amepata asilimia 48.23 ya kura.

Ali Bongo ambaye aliingia madarakani mwaka 2009 baada ya kifo cha baba yake yaani, Omar Bongo ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1967; mara hii alikabiliwa na kibarua kigumu kutoka kwa kiongozi wa upinzani Jean Ping, mwanadiplomasia mtajika wa Gabon ambaye alikuwa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kutoka mwaka 2008 hadi 2012.