Wapinzani Zimbabwe wakaidi amri ya kutoandamana
Muungano wa vyama vya upinzani Zimbabwe, NERA, umetangaza kukaidi amri ya polisi ya kupiga marufuku maandamano katika mji mkuu Harare.
Mnamo Septemba 13, Polisi ya Zimbabwe ilitangaza marufuku ya maandamano yote mjini Harare kuanzia Septemba 16 hadi Oktoba 15 wiki moja baada ya mahakama kutoa hukumu kuwa polisi inakiuka sheria katika kupiga marufuku maandamano.
Msemaji wa muungnao wa upinzani Douglas Mweonzora amesema kwa kuzingatia kuwa mahakama ilishabatilisha amri ya polisi ya kupiga marufuku maandamano, wapinzani watakaidi amri mpya ya polisi ya kutoandamana.
Katika wiki za hivi karibuni, Zimbabwe imeshuhudia maandamano ya wapinzani wanaomtaka Rais Robert Mugabe aondoke madarakani. Wapinzani wanasema Mugabe ameshindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira nchini humo. Mugabe, mwenye umri wa miaka 92 na ambaye ametawala Zimbabwe tokea ipata uhuru wake mwaka 1980 amesema atatetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018.