Jeshi la Uganda lafelisha mashambulio ya al Shabab, laua makamanda
Wanajeshi wa Uganda wanaoshiriki kwenye operesheni za kijeshi za kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM nchini Somalia wamefanikiwa kuvunja mashambulio mawili ya kundi la kigaidi la al shabab katika kambi za AU kama ambavyo wamefanikiwa pia kuua makamanda wawili wa kundi hilo katika siku chache zilizopita.
Afisa wa masuala ya habari wa wanajeshi wa Uganda nchini Somalia, Kepteni Flavia Terimulungi amenukuliwa na gazeti la New Vision la nchini Uganda akithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wiki iliyopita, al Shabab walifanya shambulio la kushitukiza la usiku dhidi ya wanajeshi wa Uganda UPDF katika eneo la Qoryooley lililoko umbali wa kilomita 120 Kusini Magharibi mwa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, lakini wanajeshi wa Uganda walikabiliana na wanamgambo hao na kuwasababishia hasara kubwa. Kepteni Terimulungi ameongeza kuwa, kamanda wa al Shabab Mohammed Farwar ambaye ndiye aliyeongoza shambulio hilo, ni miongoni mwa wanamgambo waliouawa. Amesema katika tukio jengine lililotokea mapema wiki hii, kikosi hicho cha Uganda kilishambuliwa na al Shabab katika eneo la Marka, lakini wanajeshi wa Uganda walifanikiwa kuwashinda wanambo hao na kumuua kamanda wao aliyejulikana kwa jina la Abdul Rahman Pakeli.