Kuongezeka maafa ya vita nchini Libya
Vifo vinavyotokana na mapigano ya wapiganaji wanaojiita Baraza la Kimapinduzi la Benghazi na vikosi maalumu vya Libya vimefikia watu 14.
Vyombo vya hospitali nchini humo viliripoti jana Jumamosi kwamba vita vikali vilijiri katika mji wa Benghazi ulioko mashariki mwa Libya na kupelekea watu 14 kupoteza maisha na wengine 32 kujeruhiwa. Awali ripoti zilikuwa zimesema kuwa ni mtu mmoja tu ndiye aliyekuwa amepoteza maisha katika vita hivyo na wengine watatu kujeruhiwa. Msemejai wa vikosi vinavyofungamana na serikali inayoungwa mkono kimataifa ya Libya amesema kuwa vita hivyo vilitokea katika eneo la Boatni. Jeshi la serikali hiyo linapigana na makundi ya kitakfiri katika mji huo. Kwa miaka mitano sasa Libya imekuwa ikikabiliwa na vita vya ndani ambavyo vimezuka nchini humo kutokana na kuvurugika kwa hali ya usalama iliyosababishwa na kung'olewa madarakani utawala wa dikteta Muammar Gaddafi. Hadi sasa serikali ya umoja wa kitaifa haijabuniwa nchini humo kutokana na mivutano iliyopo kati ya makundi tofauti ya kisiasa.