Kuwekwa na Marekani kambi kubwa ya kijeshi nchini Niger
Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imetenga kwa akali kiasi cha Dola milioni 50 kwa ajili ya kuibadili kambi yake ya kijeshi mjini Agadez, katikati mwa Niger na kuwa mahala pa kuhifadhia ndege zake za kivita nchini humo.
Kwa mujibu wa Michael Blunders, Msemaji wa Pentagon, kiasi hicho kinajumuisha kuanzishwa sehemu mpya ya kurukia ndege, miundombinu na kurahisisha shughuli za kijeshi katika suala hilo. Hata kama kiwango cha awali kilichotajwa kwa ajili ya shughuli hiyo ni sawa na Dola
milioni 50, hata hivyo inatazamiwa kuwa kiasi hicho kitaongezeka mara mbili zaidi ili kufanikisha mpango huo. Itafahamika kuwa, hivi sasa askari wa Marekani wapo mjini Niamey, mji mkuu wa Niger wakishirikiana bega kwa bega na askari wa Ufaransa kupitia fremu ya operesheni zao dhidi ya ugaidi, ambapo katika suala hilo wanatumia moja ya viwanja vya ndege vya nchi hiyo. Inaelezwa kuwa uwanja huo unaotumiwa na askari wa Marekani umejazwa ndege zisizo na rubani za MQ-9 za nchi hiyo. Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imezidisha uzingatiaji wake maalumu kwa bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi cha kijeshi kinachoitwa 'AFRICOM.' Amri ya kuundwa kikosi hicho ilitolewa na rais wa wakati huo wa Marekani George W. Bush, hapo Oktoba 2007, ambapo ilianza rasmi shughuli zake mwezi Oktoba mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 2008. Makao makuu ya kikosi cha AFRICOM yapo katika kambi kuu ya kijeshi ya Kelley Barracks mjini Stuttgart, Ujerumani. Kuundwa kikosi hicho kunaashiria stratijia zaidi za viongozi wa Marekani kulihusu bara la Afrika. Mtazamo wa viongozi wa usalama na kijeshi wa Marekani, mbali na kwamba unasaidia kudhamini maslahi ya Washington katika kipindi kirefu kwa ajili ya kukabiliana na kupenya madola mengine makubwa barani Afrika kama vile Uchina, inahesabiwa pia na Marekani kuwa ni hatua katika kufikia stratijia ya ushindani kupitia kile kinachotajwa kuwa ni kupambana na ugaidi. Kwa itikadi ya viongozi wa usalama nchini Marekani, hivi sasa bara la Afrika linabadilika kuelekea kuwa moja ya maeneo makuu katika kuzalisha kwa kiwango kikubwa makundi yenye kufurutu ada na ya kigaidi. Kwa hakika harakati za makundi kama vile Boko Haram na ash-Shabab, ndizo zimetoa mwanya kwa mdola ya Magharibi kutumia nara za kupambana na ugaidi, kuweza kujiimarisha kijeshi barani Afrika. Kabla ya hapo pia ilitabiriwa kuongezeka uzingatiaji wa Washington kwa bara hilo, kisiasa baada ya kijeshi na kiusalama. Kwa kuzingatia kuwa Marekani inatumia kaulimbiu ya kupambana na ugaidi ili kuhalalisha upenyaji wake barani Afrika, ndio maana Pentagon ikatumia ndege zisizo na rubani katika operesheni zake za kiupelelezi, kiujasusi na kadhalika katika kutekeleza mashambulizi ya anga katika maeneo ambayo usalama wa rubani unakuwa hatarini. Kwa kuzingatia suala hilo, tunaweza kusema kuwa, ujenzi wa miundombinu mpya ya kijeshi nchini Niger, utaongeza uwezo wa jeshi la Marekani kwa ajili ya kutekeleza mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya makundi ya wabeba silaha katika nchi jirani kama vile, Libya, Mali na hata Nigeria.
Mpango huo unahesabika kuwa mradi muhimu wa kijeshi kwa Marekani barani Afrika. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, kwa kuzingatia kufeli kukubwa kwa Washington katika mashambulizi yake ya kijeshi nchini Afghanistan na Iraq, ambayo yalipelekea kuongezeka na kuzaliwa kwa idadi kubwa ya makundi ya kigaidi eneo la Mashariki ya Kati na Asia ya kusini, hivi sasa Marekani imeelekeza zaidi nguvu zake za kijeshi na kifedha upande wa Afrika. Kwa mtazamo wa Washington, bara la Afrika ni eneo ambalo liko hatarini zaidi kukumbwa na vitendo hatari hususan mashambulizi ya kigaidi. Moja ya hatari hizo ni kuongezeka uharamia katika eneo la Pembe ya Afrika, machafuko na kadhalika kushindwa serikali kuzuia upenyaji na ongezeko la makundi ya kitakfiri kama vile al-Qaidah, Daesh, Boko Haram, Answaru Sharia na ash-Shabab.